DAR ES SALAAM: RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Wallace Karia, ametoa onyo kali kwa waamuzi wa Ligi Kuu, akisema msimu huu hautakuwa wa mzaha kwa yeyote atakayeharibu mchezo.
Akizungumza Dar Es Salaam leo kwenye makao makuu ya TFF, Karume – Ilala, wakati wa kufunga Semina ya Waamuzi wa Ligi Kuu, Karia alisema msimu huu ni tofauti na utahakikisha kila mwamuzi anafanya kazi kwa weledi na uadilifu.
“Huu ni msimu tunatarajia utakuwa tofauti sana. Tukimaliza tutapongezana, lakini kwa wale watakaokuwa tofauti tutaachana nao moja kwa moja na wala hilo sitanii,” alisema Karia.
Karia alibainisha kuwa kutakuwa na jopo la waamuzi watakaokuwa wakijadili matukio ya ligi, na kamati ya waamuzi itashirikiana na vyombo vya serikali pale inapobidi kuhakikisha haki inatendeka.
“Kwa hali halisi ilivyokwenda msimu uliopita, ilikuwa ni mtikisiko mkubwa kwa nchi, mliitikisa serikali. Hivyo taasisi za serikali pia zitahusishwa,” aliongeza.
Hata hivyo, Karia aliwatia moyo waamuzi akisema wana uwezo na ujuzi mkubwa wa kutafsiri sheria, hivyo hawapaswi kuwa chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo ya soka la Tanzania.
“Mpira wetu tumeufikisha sehemu kubwa sana, sehemu ambayo dunia nzima inatutambua sasa hivi. Kwa hiyo tusiwe chanzo cha kuporomoka,” alisisitiza.
The post Karia: Hatutavumilia uzembe wa waamuzi msimu ujao first appeared on SpotiLEO.