DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Kriketi ya Tanzania imerejea jijini Dar es Salaam baada ya kampeni ya kuvutia katika mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia la ICC Women’s T20 Kanda ya Afrika.
Wakiwa wamepata ushindi katika michezo minne kati ya mitano, ikiwemo kuichapa Uganda mara mbili licha ya kuwa na nafasi ya juu katika viwango, kikosi hicho kimekamilisha safari yake kwa kumaliza nafasi ya tatu barani Afrika.
Hatua hiyo imeonesha wazi kuwa kriketi ya wanawake nchini ipo kwenye mwanga mpya na ina mustakabali mzuri.
Mapokezi yao yamefanywa na Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), Dk Balakrishna Sreekumar, mchujuaji wa timu ya taifa Adil Kassam pamoja na gwiji wa mchezo huo, Viru Kamania ambao waliipongeza timu hiyo kwa kufanya vizuri.
Wachezaji hao sasa wanatarajiwa kwenda likizo ya wiki mbili kabla ya kurejea mazoezini kwa maandalizi ya mchezo muhimu dhidi ya Canada utakaopigwa Oktoba 27.
“Wameonesha ari, mshikamano na kujituma kwa kiwango cha hali ya juu. Ni fahari kubwa kwa taifa,” alisema Dk. Sreekumar.
The post Kriketi wanawake warejea baada ya kung’ara Afrika first appeared on SpotiLEO.