NEWCASTLE: MSHAMBULIAJI wa Barcelona Marcus Rashford alikuwa kwenye kiwango bora jana usiku wakati mabingwa hao wa LaLiga walipokuwa wageni wa Newcastle United kwenye Dimba la St James Park katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Fowadi huyo wa zamani wa Manchester United aliyeko kwa mkopo klabuni hapo alifunga mabao yake mawili ya kwanza kwa timu yake hiyo mpya. Mabao ambayo yalisaidia Barcelona kuanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa kwa kushinda 2-1 dhidi ya Newcastle.
Rashford alifunga bao la kwanza dakika ya 58 baada ya Kwenda hewani na kujitwisha mpira Jules Koundé, kisha kuzama kwenye nyavu za Nick Pope aliyekosa la kufanya na nyavu zake kutikisika.
Dakika tisa baadaye rashford alirudi tena kwa Pope, safari hii akitumia mpira uliotua kwake kwa makosa ya mchezaji wa Newcastle kisha kumtesa kipa huyo kwa shuti kali la nje ya 18 na kuwafanya wakatalan hao kuondoka na pointi 3 England.
“Mambo yanaenda vizuri hapa (Barcelona), ninajifunza mbinu mpya zinazonifanya kuwa bora kila siku. Ni jambo zuri kuichezea Barcelona na tunataka kushinda mechi nyingi kadri tuwezavyo. Inafurahisha kucheza Pamoja na hawa watu.” – Rashford alisema
Beki wa Barcelona Ronald Araujo alisema Rashford amekuwa kivutio muda wote wa mechi akiongeza kuwa uwezo wake hauna mashaka kwani wamekuwa wakiuona kila siku kwenye mazoezi akienda mbali na kusema kuwa ameichangamsha timu hiyo na wana furaha kuwa nae.
Rashford alijiunga na Barcelona kwa mkopo wa msimu mzima mwezi Julai baada ya mabingwa hao wa Hispania kushindwa kumnasa winga Nico Williams kutoka Athletic Bilbao.
Aliwahi kutajwa miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu barani Ulaya, lakini miaka ya karibuni mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alipitia wakati mgumu baada ya kupoteza Imani ya kocha wa United Ruben Amorim na kumaliza msimu uliopita kwa mkopo Aston Villa.
The post Rashford aanza kazi rasmi Barca first appeared on SpotiLEO.