SEVILLA: KLABU ya Nottingham Forest ya Ligi kuu ya England inarejea kwenye mashindano ya Ulaya baada ya miongo mitatu na safari ya kwenda Hispania kumenyana na Real Betis katika mechi ya ufunguzi wa Europa League leo Jumatano.
Mara ya mwisho timu hiyo ya Ligi Kuu ya England kuwa katika michuano ya ulaya ilifika robo fainali ya Kombe la UEFA wakati huo, mashindano ambayo sasa yanajulikana kama UEFA Europa League, katika msimu wa 1995/96 na haijarejea tena tangu wakati huo.
Forest bado inasaka ushindi wake wa kwanza chini ya kocha mpya Ange Postecoglou baada ya kupoteza mara mbili na sare moja tangu meneja huyo wa zamani wa Tottenham achukue mikoba ya Nuno Espírito Santo aliyetimuliwa.
Postecoglou alifutwa kazi na Tottenham mwezi Juni licha ya kutwaa taji la Europa League taji la kwanza la Spurs ndani ya miaka 17 baada ya msimu ambao walikuwa na kampeni yao mbaya zaidi ya Ligi, wakimaliza nafasi ya 17.
Forest wapo Europa League badala ya Crystal Palace, mshindi wa Kombe la FA la England baada ya kushushwa na UEFA katika kesi tata inayohusiana na wamiliki wa klabu hiyo kuwa na hisa katika Klabu nyingi. Crystal Palace itacheza Conference League.
Katika michezo mingine ya Europa League leo Jumatano, AS Roma itaanzia Nice, Freiburg ya Bundesliga ikiwakaribisha mabingwa wa Uswizi FC Basel, Feyenoord watasafiri kwenda Braga, Celtic wanakutana na Red Star Belgrade na PAOK inacheza na Maccabi Tel-Aviv nyumbani. Michezo tisa iliyosalia imepangwa kufanyika Alhamisi.
Europa League inatumia muundo sawa wa ligi ya timu 36 kama Ligi ya Mabingwa. Timu hucheza na wapinzani nane tofauti na kuorodheshwa katika jedwali la msimamo mmoja.
The post Forest kuanza kampeni UEL leo first appeared on SpotiLEO.