BARCELONA: KIUNGO wa Barcelona Pablo Gavi amewatumia ujumbe wa matumaini mashabiki akiwa kwenye kitanda cha hospitalini, huku akiwa amezungukwa na wachezaji wenzake, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kutibu jeraha la meniscus katika goti lake la kulia.
Gavi alichapisha picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akionesha dole gumba Pamoja na wachezaji wenzake Lamine Yamal, Ronald Araujo na Pedri wakiwa wamesimama karibu na kitanda chake cha hospitali.
“Mnaonijua mnajua kwamba nitarudi haraka iwezekanavyo kuitetea Barça na wachezaji wenzangu hadi mwisho. Bingwa wa kweli haonekani wakati wa mafanikio pekee, bali katika nyakati ambazo huinuka baada ya kuanguka. Nawashukuru nyote kwa jumbe za kutia moyo na upendo!” – chapisho hilo lilisema
Gavi alifanyiwa upasuaji Jumanne na Barcelona ilisema muda wake wa kupona utakuwa kati ya miezi minne hadi mitano. Uamuzi huo ukifanywa baada ya Gavi kufanyiwa vipimo vya kina vinavyofutatiwa na matibabu zaidi.
Gavi ameichezea Barcelona mechi mbili pekee msimu huu, zote mwezi Agosti.
The post “Nitarudi haraka kuitetea Barca” – Gavi first appeared on SpotiLEO.