LONDON: mshambuliaji mpya wa Manchester United Bryan Mbeumo atakuwa na hisia mseto ikiwa mchezaji huyo wa zamani wa Brentford atafunga bao kwenye mechi yake ya kwanza kwenye uwanja wa nyumbani wa klabu yake ya zamani wa Community Stadium kwenye EPL Jumamosi.
Inawezekana asishangiliwe sana na mashabiki wa Brentford ikiwa atafunga lakini ni wazi hakutakuwa na kuzomea pia kutoka kwa mashabiki ambao ana uhusiano nao wa kipekee.
Mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa na ushirikiano mzuri na Yoane Wissa ambaye pia hayupo kikosini hapo, alijiunga na United mwezi Julai kwa pauni milioni 65 na tayari amefungua akaunti yake ya mabao kwenye ligi.
Tofauti na Wissa, ambaye alijiunga na Newcastle United baada ya mvutano mkali na Brentford na kuonekana waziwazi akitaka kuhama, Mbeumo aliondoka katika kabu hiyo ya Magharibi mwa London bila shida yeyote akiuacha salama uhusiano wake na mashabiki.
Alifunga mabao 70 katika mechi 242 katika kipindi cha miaka sita akiwa ndani ya ‘uzi’ wa Brentford hata akatayarisha video ya kuwaaga mashabiki alipoondoka.
Hakutakuwa na’sapraizi’ katika mechi hiyo ya mapema, kwani si Brentford au United aliyeanza vyema msimu huu. Brentford wanaelea juu kidogo tu ya nafasi za kushuka daraja katika nafasi ya 17 na Manchester United wakizagaa katika nafasi ya 11.
United iliifunga Chelsea mabao 2-1 Uwanjani Old Trafford wikendi iliyopita, ukiwa ni ushindi wao wa pili msimu huu, lakini hawajashinda mechi mfululizo za ligi tangu Mei mwaka jana na bado hawajashinda ugenini.
Brentford wameshinda mechi mbili kati ya tatu za mwisho walizokutana na United nyumbani, ingawa sasa wako chini ya kocha mpya Keith Andrews kufuatia Thomas Frank kuhamia Tottenham Hotspur.
The post Hisia kali Mbeumo akirejea Brentford first appeared on SpotiLEO.