Baada ya matokeo yasiyoridhisha katika michezo ya hivi karibuni kati ya Yanga na Mbeya City, sintofahamu juu ya hatma ya kocha mkuu wa Yanga SC, Romain Folz, imeendelea kuchukua nafasi kubwa katika mijadala ya wapenzi wa soka nchini. Taarifa zinazosambaa zinaonyesha kuwa uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukitafakari hatua za kuchukua kuhusu mustakabali wa kocha huyo, huku Ahmed Ally akidai kuwa kikao maalum kilifanyika mkoani Mbeya kujadili suala hilo.
Msemaji wa Simba FC, Ahmed Ally, alidai kuwa viongozi wa klabu hiyo walikutana kwa dharura mara tu baada ya mechi iliyochezwa Mbeya, wakijadili namna bora ya kumaliza mkataba na Folz kutokana na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha. Lakini pia mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakiinba nyimbo mbalimbali zilizopeleka ujumbe wa moja kwa moja kuwa hatumtaki kocha.
Hata hivyo, taarifa ya kikao cha siri imepingwa na kauli iliyotolewa hivi karibuni na msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, ambaye alikanusha kuwepo kwa kikao chochote cha kumjadili kocha huyo. Akizungumza na waandishi wa habari, Kamwe alisema, “Hakuna kikao walichokaa viongozi wa Yanga kumjadili kocha baada ya mechi ya jana.”
Kauli hizi mbili zinazokinzana zimeibua maswali mengi kuhusu hali halisi ndani ya klabu hiyo kongwe. Baadhi ya wachambuzi wa soka wanasema kuwa kauli ya Kamwe huenda ni mbinu ya kupunguza presha kutoka kwa mashabiki wakati uongozi ukiendelea kupanga mikakati ya mabadiliko kimyakimya.
Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakilalamikia mwenendo wa timu chini ya Folz, wakimtuhumu kwa kushindwa kuleta matokeo ya kuridhisha licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye kikosi. Mengi yanatarajiwa kujulikana katika siku chache zijazo, huku mashabiki wakiwa na shauku kubwa kuona kama uongozi utamwacha kocha huyo aendelee au atapisha nafasi kwa mtu mwingine.
Iwapo sauti ya mashabiki wa Yanga itapewa uzito, basi huenda hatma ya Romain Folz ikawa mashakani zaidi kuliko ilivyokuwa ikidhaniwa awali. Muda pekee ndio utaamua mustakabali wa benchi la ufundi la Yanga SC.