MANCHESTER: HALI inazidi kuwa tete kwa kocha wa Manchester United, Ruben Amorim, ambaye hadi sasa ameonekana kutokuwa na presha na kibarua chake Old Trafford licha ya takwimu kumsimanga hadharani na kuzua hasira kwa mashabiki.
Amorim amevuna pointi 34 pekee katika mechi 33 za kwanza kwenye Ligi Kuu ya England, rekodi mbaya zaidi kwa meneja yeyote wa United tangu kustaafu kwa Sir Alex Ferguson mwaka 2013. Tangu wakati huo, makocha watano wa kudumu kuanzia David Moyes hadi Erik ten Hag, wote walikusanya angalau pointi 56 katika idadi hiyo hiyo ya michezo.
Kwa kiwango cha wastani wa chini ya pointi moja kwa mchezo, United ipo kwenye hatari ambayo zamani ingeashiria kushuka daraja katika historia ya Ligi Kuu. Ingawa jumla ya pointi zinazohitajika kuwa salama imekuwa ikipungua katika misimu ya karibuni, mwenendo wa Amorim bado unaibua maswali mengi.
“Matokeo haya ni mabaya sana kwa Manchester United, Fedha zilizowekezwa ni kubwa mno, lakini bado kuna mambo yanayoibua wasiwasi mkubwa, baadhi yake hayapaswi hata kutokea.” – alisema nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Gary Neville, kupitia Sky Sports.
Mshambuliaji wa zamani wa United, Wayne Rooney, pia alionesha wasiwasi wake kwenye podikasti yake, akirejelea kipigo cha mabao 3-1 cha hivi karibuni kutoka Brentford wiki iliyopita.
“Kwa kweli natumai ataweza kubadili hali hii, Lakini ukiuliza kama nina imani naye katika kufanya hivyo, baada ya kila nilichoshuhudia, kwa kweli sioni matumaini yeyote.” alisema Rooney
The post Takwimu zamkataa Amorim United first appeared on SpotiLEO.