ALGIERS: MTOTO wa nyota wa soka wa Ufaransa Zinedine Zidane ambaye pia ni golikipa wa Granada ya Hispania Luca Zidane amejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Algeria kwa mara ya kwanza baada ya kuamua kuitumikia timu hiyo badala ya Ufaransa wakati huu Algeria wakijiandaa kwa mechi muhimu za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026.
Luca Zidane, mwenye umri wa miaka 27, amekuwa akiiwakilisha Ufaransa katika ngazi ya timu za vijana lakini hakuwahi kuichezea timu ya taifa ya wakubwa amepata nafasi hiyo ya kuiwakilisha Algeria kupitia uhusiano wa kinasaba wa familia ya baba yake.
FIFA iliidhinisha ombi la mabadiliko hayo ya utaifa wiki mbili zilizopita kwa Luca Zidane, ambaye aliwahi kucheza Real Madrid wakati baba yake alipokuwa kocha wa mabingwa hao wa kihistoria wa UEFA Champions League.
Kocha wa Algeria Vladimir Petkovic amemjumuisha Luca katika kikosi chake cha wachezaji 26 kwa ajili ya michezo ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Somalia Oktoba 9 na Uganda siku tano baadaye.
Algeria inaongoza kundi la kufuzu kwa tofauti ya pointi nne dhidi ua Uganda walio katika nafasi ya pili na ushindi katika mechi hizo mbili utaipeleka timu hiyo moja kwa moja kwenye Kombe la Dunia linaloandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico.
Algeria imecheza makala nne za Kombe la Dunia la wanaume na kufika hatua ya 16 mara ya mwisho katika 2014.
Zinedine Zidane aliichezea Ufaransa Kombe la Dunia mara tatu, na kushinda taji la 1998 nyumbani na kupoteza fainali mwaka 2006. Kadi yake nyekundu katika muda wa ziada wa fainali ya 2006 kwa kumpiga kichwa beki wa Italia Marco Materazzi ni sehemu ya historia ya Kombe la Dunia na ulikuwa mchezo wake wa mwisho akiwa mchezaji.
The post Zidane aitwa timu ya taifa Algeria first appeared on SpotiLEO.