Nimeangalia kiwango chake cha msimu huu naona kimeendelea pale alipoishia katika msimu uliopita. Hajakuwa na maajabu mengi. Hana maamuzi mazuri. Na katika kitu ambacho nimekuwa nikimlaumu Mpanzu tangu msimu ulioisha ni mbinafsi uwanjani. Sidhani kama anacheza sana kwa ajili ya timu.
Wakati mwingine juhudi zake binafsi zimekuwa zikiiisaidia Simba, lakini wakati mwingine anahitajika kurahisisha maisha kwa wengine kwa sababu ana kipaji kikubwa. Hili huwa halifanyi mara nyingi lakini kama akili yake ya kwanza ingekuwa kuwasaidia wenzake uwanjani basi wachezaji wengi wa Simba eneo la mbele wangekuwa wananufaika na Mpanzu.
Na kwa sasa wakati hatumwelewi vizuri Mpanzu ni vyema kumkumbusha kuna watu waliishika Simba vizuri zaidi yake. Kuna mmoja alikuwa Mganda mwingine alikuwa anatoka Msumbiji na mwingine anatoka Zambia. Waliishika Simba vyema kiasi walistahili kuringa katika siku za baadae. Kuna huyu Mganda Emmanuel Okwi. Aliishika Simba vema kiasi kwamba mashabiki na viongozi walikuwa hawapumui juu yake. Waliishiwa pawa kwa mapenzi dhidi yake. Okwi kwa Simba alikuwa kama Diego Maradona na Argentina ya mwaka 1986 katika fainali za Kombe la Dunia pale Mexico. Alikuwa na mpango wake wa mtu mmoja. Mechi nyingi alikuwa anaamua yeye mwenyewe bila ya kuhusisha watu wengine.
Baadaye wakaja Mmakonde Jose Luis Miquissone na Mzambia Clatous Chama. Hawa pia waliishika Simba ikitamba robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika. Mpanzu bado hajaishika Simba kiasi hicho. Mpanzu apambane kuipeleka Simba inakostahili. Wamekuja kina Seleman Mwalimu, Morice Abraham, Jonathan Sowah na wengineo. Wanaweza kuwa wachezaji wazuri kuliko wale aliokuwa nao msimu uliopita.
Ufalme wa miezi mitatu tu ambao aliutengeneza alipowasili unaweza kupotea kama akiendelea na kiwango hiki. Tusirudi kwa kina Okwi na Chama, amtazame tu hata Pacome ambaye wiki baada ya wiki ameendelea kuwa mchezaji yule yule tu.
Vinginevyo wengine tutamchukulia Mpanzu kama Big G. Ukianza kuitafuna inakuwa tamu, lakini kadri ikiendelea kuwa mdomoni utamu unaondoka. Alianza vizuri haswa, lakini kadri tunavyosonga mbele anageuka kuwa mchezaji wa kawaida. Utamu wake unapotea.
— LEGEND, Edo Kumwembe