DAR ES SALAAM:HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga SC, ni kurejea kwa nyota wao Clement Mzize na Yao Kouassi mazoezini baada ya muda wa kuwa nje kutokana na majeraha.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ally Kamwe, amesema kurejea kwa wachezaji hao ni ishara kuwa timu inazidi kuimarika kadiri siku zinavyokwenda, huku akisisitiza kuwa maandalizi kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi yanaendelea vizuri.
“Timu yetu imeanza kunoga. Yao Kouassi na Clement Mzize wameanza mazoezi na hali ni nzuri. Kadiri siku zinavyokwenda tutakuwa imara zaidi,” alisema Kamwe.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa madaktari, Yao anatarajiwa kurejea dimbani rasmi mwezi Novemba, jambo linaloleta matumaini makubwa kwa benchi la ufundi na mashabiki wa Yanga.
Kamwe pia ametoa wito kwa mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kusafiri kwenda Malawi kuisapoti timu yao, akibainisha kuwa tayari magari 15 yameandaliwa kwa safari hiyo.
“Kiu ya mashabiki kwamba tunashinda na tunapiga mpira mwingi inaendelea. Kwa hiyo tusafirini twendeni Malawi, tukaiunge mkono timu yetu,” alisema Kamwe.
Yanga inatarajiwa kukabiliana na Silver Strikers katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa nchini Malawi, ikiwa na azma ya kupata matokeo chanya na kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya kimataifa.
The post Mzize na Yao warejesha matumaini Yanga first appeared on SpotiLEO.