KUNA mambo mawili Simba inakabiliana nayo leo Jumapili inapoikaribisha Nsingizini Hotspurs kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mechi ya marudiano ya hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu makundi.
Jambo la kwanza ambalo Simba inakabiliana nalo, ni kuimarisha rekodi yake ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya CAF ikiwa tayari imefanya hivyo mara tano mfululizo, ikiwa ndiyo klabu ya Tanzania iliyofika hatua hiyo mara nyingi.
Ukiweka kando hilo, pia licha ya kushinda ugenini 3-0 dhidi ya Nsingizini ya Eswatini, inapaswa kujipanga kutojirudia kilichowahi kuwakuta msimu wa 2021–2022 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoaibishwa nyumbani licha ya ugenini kushinda 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Msimu huo, Simba ilirudiana na Jwaneng Galaxy ikiwa na mtaji wa mabao 2-0, lakini ikafungwa 3-1 nyumbani na kutupwa nje ya michuano hiyo, kwa bahati nzuri, ikaangukia mtoano na kufuzu makundi Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa sasa, sheria zimebadilika, ukipigwa, ndio moja kwa moja, hakuna kupewa nafasi nyingine ya kujiuliza.
Simba leo inaingia uwanjani ikiwa na matumaini ya kushinda na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo ambapo Meneja Mkuu, Dimitar Pantev sambamba na kocha Seleman Matola, wana kazi ya kuwapa burudani Wanasimba na Watanzania kwa ujumla.
Ushindi wa Simba, utamaanisha kwamba, timu hiyo inakwenda kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa msimu wa sita mfululizo, lakini pia itakuwa ni msimu wa saba katika miaka minane ya hivi karibuni tangu 2018-2019.
Kocha wa Simba, Selemani Matola na nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe, wametamba kuendelea kufanya vizuri katika mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Nsingizini Hotspurs.
Matola amesema licha ya ushindi mzuri katika mechi ya kwanza, lakini hawatabweteka kwa sababu wanahitaji kufunga mabao mengi zaidi na kufuzu kwa kishindo.
“Ni kweli tuna uzoefu mkubwa katika hii michuano, lakini hatutaki kurudia kile kilichowahi kutukuta misimu kadhaa nyuma, hii ni mechi nyingine yenye uhitaji mkubwa kama ilivyokuwa ile ya mwanzoni ugenini,” amesema.
Simba inakwenda uwanjani leo ikiwa imetoka kutajwa kuwa kati ya klabu kumi zinazowania tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka 2025 katika Tuzo za CAF ambapo Matola amesema hilo linawaongezea motisha ya kufanya vizuri zaidi.
“Sio kwa bahati mbaya sisi kupata hiyo nafasi kwa sababu ni kutokana na mafanikio ambayo tumekuwa nayo ya kimataifa, kwetu inatupa morali ya kuzidi kupambana katika michuano hii mikubwa barani Afrika,” amesema.
Akizungumzia hali ya wachezaji wa timu hiyo, Matola amesema beki wa kikosi hicho, Wilson Nangu aliyepata majeraha katika mechi ya kwanza, yupo fiti kucheza huku kiungo mshambuliaji, Mohamed Bajaber akiendelea vizuri baada ya kupewa programu maalumu.
Nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe, amesema licha ya ushindi katika mechi ya kwanza, wao kama wachezaji wamejipanga vizuri kuendeleza kiwango bora zaidi.
“Niwaombe mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwa sababu mechi za kwanza hawakupata hiyo nafasi, hii ni fursa nyingine nzuri ya kuendelea kuandika historia mpya kwa umoja wetu.
“Nina majukumu mazito kama nahodha wa kuipelekea Simba mbali zaidi ya hapa, naamini kwa umoja na ushirikiano wetu tutafikia malengo ambayo tumedhamiria kwa msimu huu,” amesema Kapombe.
MATUMAINI YA NSINGIZINI
Kocha Mkuu wa Nsingizini Hotspurs, Mandla Qhogi, amesema licha ya kikosi hicho kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Simba katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wana nafasi ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Mandla amesema anatambua ugumu uliopo wa kushinda ugenini kwa zaidi ya mabao matatu, ingawa katika mpira wa miguu kila kitu kinawezekana.
“Kabla ya mechi yetu ya kwanza hakuna aliyetarajia pia kama Simba ingeshinda ugenini kwa idadi kubwa ya mabao, hii ni mechi nyingine ngumu ila tutapambana kadri ya uwezo wetu,” amesema.
Aidha, Mandla amesema licha ya ugumu wa kupindua matokeo ya kwanza, watapambana kwa ajili ya Taifa lao na mashabiki wa eSwatini.
“Unapotaja kati ya timu tano bora Afrika huwezi kuiacha kuitaja Simba, tunatambua tunaenda kucheza kwenye uwanja wenye uwezo mkubwa wa kubeba mashabiki zaidi ya 60,000, hivyo, tuna kazi pia ngumu ya kufanya ili tusonge hatua inayofuata,” amesema Qhogi.
Nyota wa Nsingizini, Khanyakwezwe Shabalala, amekiri deni kubwa wanalokabiliana nalo kama wachezaji, ingawa sio kigezo cha kucheza kwa presha zaidi wakiwa ugenini.
“Tumefanyia kazi udhaifu mkubwa tulioonyesha katika mechi yetu ya kwanza, hususani kuwaruhusu wapinzani wetu kutushambulia kwa kutushtukiza,” amesema Shabalala.
REKODI YA MAKUNDI
Simba katika safari ya kucheza hatua ya makundi michuano ya CAF mara sita kipindi cha miaka saba iliyopita, imekuwa mikononi mwa makocha sita tofauti walioweka rekodi hiyo, akiwamo mzawa mmoja Juma Mgunda.
Baada ya kupita miaka mingi, Simba ilianza kwa kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019 ikiwa inafundishwa na kocha Patrick Aussems.
Katika mechi iliyoipeleka Simba hatua ya makundi, iliifunga Nkana jumla ya mabao 4-3, kufuatia mechi ya kwanza kupoteza ugenini kwa mabao 2–1, kisha nyumbani Simba ikashinda 3–1.
Baada ya hapo, 2019-2020, haikufika makundi, lakini kuanzia hapo, suala la Simba kucheza hatua ya makundi michuano ya CAF kwa maana ya Kombe la Shirikisho au Ligi ya Mabingwa, limekuwa ni jambo la kawaida.
Sven Vandenbroeck aliipeleka Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020–2021 baada ya kuiondosha FC Platinum kwa jumla ya mabao 4-1. Licha ya mechi ya kwanza ugenini kupoteza kwa bao 1–0, ikarudi nyumbani na kuiangushia mvua ya mabao 4–0.
Kidogo Simba iliteleza msimu wa 2021-2022 katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikashindwa kufuzu makundi ikiwa chini ya Thierry Hitimana ambapo timu hiyo ilishinda ugenini 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, nyumbani ikachapwa 3-1, ikatolewa kwa kanuni ya bao la ugenini matokeo ya jumla yakiwa 3-3.
Simba ikaangukia mtoano kucheza kuwania kufuzu makundi upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, ndipo kocha Pablo Franco Martin akakabidhiwa kikosi huku Hitimana akiwa msaidizi, timu ikafanya kweli kwa kufuzu makundi Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021–2022 ikiiondosha Red Arrows kwa jumla ya mabao 4-1. Simba ilianzia nyumbani ikishinda 3–0, ugenini ikaenda kuchapwa 2–1.
Juma Mgunda anaingia kwenye rekodi ya kuipeleka Simba makundi upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa msimu wa 2022–2023 ambapo alikabidhiwa kikosi kwa muda ikiwa ni baada ya kuondoka kwa Didier Gomes De Rosa.
Mgunda aliiongoza Simba kushinda ugenini mabao 1–3 dhidi ya 1º de Agosto, nyumbani Simba ikashinda tena 1–0, ikafuzu kwa jumla ya mabao 4-1.
Roberto Oliveira ‘Robertinho’ naye aliipeleka Simba makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023–2024 kwa kuitoa Power Dynamos kwa bao la ugenini, mechi ya kwanza ugenini matokeo yalikuwa 2–2, nyumbani 1–1.
Fadlu Davids akaja kufunga kazi, msimu wa 2024-2025 akaipeleka Simba makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akiifunga Al Ahli Tripoli jumla ya mabao 3–1. Ugenini matokeo yalikuwa 0-0, nyumbani Simba ikashinda 3–1.
MTIHANI ULIOBAKI
Wakati ndani ya miaka saba iliyopita Simba ikitinga hatua ya makundi ya michuano ya CAF mara sita, huku tano kati ya hizo ikiwa mfululizo, Pantev na Matola wana mitihani miwili, kisha kuandika rekodi mpya.
Mitihani waliyonayo wataalamu hao ni kuiongoza Simba kufuzu makundi kwa mara ya saba, ikiwa ni sita mfululizo, lakini pia kama kawaida kuvuka hatua hiyo na kucheza robo fainali.
Rekodi zinaonyesha Simba inapofanikiwa kuvuka kucheza hatua ya makundi michuano ya CAF, haijawahi kuishia hapo, lazima icheze robo fainali.
Msimu uliopita 2024-2025, Fadlu alivunja rekodi ya Simba kuishia robo fainali baada ya kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikapoteza mbele ya RS Berkane.
Pantev na Matola wamepewa jukumu la kuiongoza Simba baada ya Fadlu kuondoka. Sasa wanapaswa kuivusha kucheza makundi, kisha robo fainali, baada ya hapo, iende nusu fainali, kwani upande wa Ligi ya Mabingwa Simba imecheza makundi mara nne na haijawahi kuvuka zaidi ya robo fainali. Ikivuka safari hii, ni rekodi mpya.
Kubwa zaidi, Wanasimba wanataka kuona timu yao ikibeba ubingwa wa CAF, hivyo kitendo cha kucheza fainali msimu uliopita, haitakuwa na jipya tena Simba ikifika hapo na kutobeba ubingwa, rekodi mpya ni ya kuwa mabingwa wa Afrika.
Pantev amesema: “Kwa sasa hatutakiwi kuona tayari tumefika hatua ya makundi, tunatakiwa kusahau matokeo ya mechi ya kwanza, ile ilikuwa ni nusu ya safari, tunatakiwa kumaliza kazi kwa kufanya vizuri pia kwenye mechi ya marudiano.
“Tumekuwa na mazoezi tofauti yaliyolenga kuboresha kiwango chetu ili tuwe kwenye ubora ambao utatufanya kutimiza kile ambacho tunahitaji.”
WANIGERIA KUSIMAMIA SHOO
Mwamuzi wa Nigeria, Grema Mohamed amepewa jukumu la kusimamia sheria 17 za soka, katika mechi hii. Wasaidizi wake ambao wote wanatokea Nigeria ni Teejir Basmat, Emmanuel Omala na Abusalam Abiola (Mwamuzi wa mezani).
The post SIMBA vs NSINGIZINI…HAYA HAPA MAMBO MAWILI MAKUBWA…WANIGERIA KUSIMAMIA SHOW… appeared first on Soka La Bongo.






