Kocha Mkuu wa Fountain Gate Princess, Noah Kanyanga amefariki dunia jana usiku jijini Dodoma baada ya kuugua ghafla.
Akizungumza na Mwananchi Ofisa Habari wa timu hiyo, Issa Mbuzi alisema Kanyanga alikuwa na changamoto ya kiafya iliyomsababishia kuugua ghafla na alipopelekwa hospitali usiku akafariki.
Mbuzi aliongeza kuwa taratibu za msiba zinafanyika leo na watasafirisha kuelekea Mburahati Dar es Salaam na mambo ya mazishi watafahamu baada ya kufika huko.
“Jana jioni alifanya mazoezi na timu na alionekana hana changamoto yoyote, saa 12 jioni hali ilibadilika na alipopelekwa hospitali hakuchukua muda mrefu akafariki.
“Mambo yakikamilika mapema leo tutasafirisha mwili kuupeleka Mburahati ambako ndio kuna ndugu zake mambo mengine ya mazishi tutafahamu kwa familia.”
Kabla ya kuitumikia Fountain, Kanyanga aliwahi kuzifundisha JKU Princess ya Zanzibar iliyotoka kushiriki mashindano ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika, Mburahati Queens, Gets Program, Ceasiaa Queens na JMK Youth Park.
Ni miongoni mwa makocha waliokuwa na mchango mkubwa kwenye soka la wanawake na ndiye alitoa nyota kadhaa waliokuwa tegemeo kwa Simba Queens, Yanga Princess na timu nyingine hadi timu ya taifa.
Miongoni mwa nyota aliowafundisha ni mshambuliaji wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, ‘Twiga Stars’, Mwanahamis Omary ‘Gaucho’, Maimuna Hamis ‘Mynaco’, Janeth Pangamwene na wengineo.
WADAU WAMLILIA
Balozi wa Soka la Wanawake, Salva Mkindiko alisema Kanyanga alikuwa na matumaini makubwa msimu huu afanye vizuri kwenye ligi ya wanawake.
“Hivi karibuni nimekuwa nikizungumza naye sana ananiambia tunataka kuirudisha Fountain ile yenye ushindani alikuwa na matamanio makubwa sana ila kiukweli nimeumia na sijaamini hadi nimzike,”
“Juzi nimeongea naye kuna mchezaji alikuwa ananiambia nashangaa napewa taarifa jana usiku alikuwa anaangalia mechi ya Yanga na Silver Strikers amefariki dunia, hakika tutamkumbuka ni kocha alikuwa na maono makubwa sana.”
The boy meets a dog on the street – no one expected what happened next.
Women’s Method
by TaboolaSponsored Links
Elias Ilomo wa Singida Warriors alikuwa chimbuko la mwanzo la soka la wanawake.
“Daaah!, Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake. Kiufupi naweza kusema Noah ndiye chimbuko la mwanzo kabisa la Singida Warriors kushiriki mashindano makubwa kwani mwaka 2018 wakati tunaanza kushiriki ligi daraja la kwanza tulitumia wachezaji zaidi ya tisa kutoka JMK.
“Nakumbuka tulicheza mashindano yale tukiwa na mashabiki kutokea Dar es Salaam na ndio tulitengeneza msingi wa kutumia wachezaji chipukizi kwenye mashindano kwani wachezaji wote hao ilikuwa ndiyo mashindano yao ya kwanza makubwa ukitoa Umisseta na Umitashumta.”
Kiungo wa Yanga Princess, Mynaco alisema Kanyanga alikuwa kama mlezi wao na sio kocha pekee kutokana na kupambania malezi ya kila mchezaji akitamani wengi wao wafike mbali.
“Alikuwa na moyo wa kipekee sana sisi bila yeye sidhani kama hata mpira tungecheza maana alitutengeneza Mburahati Queens tukawa wachezaji muhimu sana, Mungu ampe pumziko jema.”










