ISMAILIA: KLABU ya soka ya wanawake JKT Queens tayari imetua katika mji wa Ismailia nchini Misri kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza kesho.
JKT Queens imesema safari hii wana kila sababu ya kupambana na kurejea na ubingwa kwa kuwa wanaokutana sio wazoefu kama wao.
Mratibu wa timu ya JKT Queens, Esther Ryoba, amesema malengo makuu ya kikosi hicho katika msimu huu ni kutwaa ubingwa wa Afrika baada ya kushindwa msimu wa 2023 nchini Ivory Coast ambapo waliishia hatua ya makundi.
Ryoba alisema kuwa JKT Queens wamejipanga kwa kila namna kuhakikisha wanarejea nyumbani na kombe hilo, wakiamini maandalizi mazuri na uzoefu walioupata mwaka uliopita vitakuwa nguzo yao kuu ya mafanikio.
“Safari hii JKT Queens tumekuja kuchukua ubingwa. Hii ni mara ya pili tunashiriki, tulijifunza tulipokosea mwaka jana, sasa tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafika mbali na kuchukua kombe,” alisema.
“Timu nyingi zinazoshiriki michuano hii kwa sasa ni mara yao ya kwanza, lakini sisi tunakuja kwa mara ya pili hiyo ni fursa kubwa. Tuna kikosi imara, wachezaji wenye uzoefu, na morali ya hali ya juu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, JKT Queens wataanza kampeni zao Jumapili hii, kwa kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Gaborone United ya Botswana, katika uwanja wa Ismailia nchini humo.
The post JKT Queens mguu sawa Afrika first appeared on SpotiLEO.





