Klabu ya JKT Tanzania iliyowakaribisha Simba SC kwa maneno makali kabla ya mchezo, ikiwemo kuahidi kuwa Wekundu wa Msimbazi “hawatatoka salama” katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, imejikuta ikiondoka uwanjani hapo ikiwa na hasara ya pointi tatu.
Katika mchezo uliochezwa jana, Simba SC walifanikiwa kushinda kwa mabao 2-1, ushindi uliokuja kama majibu ya moja kwa moja kwa kauli za JKT zilizowahi kuenea mitandaoni muda mfupi kabla ya mchezo.
JKT Tanzania walikuwa wanajivunia matokeo yao ya hapo nyuma dhidi ya Azam FC, ambapo walitoka sare ya 1-1, na kuamini kuwa na wao pia wangeweza kuidhibiti Simba katika uwanja huo. Hata hivyo, hali ilienda tofauti baada ya Simba kuonyesha uimara wao na kufanikiwa kuzinyakua pointi zote 3 kutoka kwa JKT Tanzania.
Ushindi huu unawafanya Simba kuendelea kujikusanyia pointi muhimu katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku JKT wakirejea kupanga hesabu zao kwenye mchezo ujao baada ya mkwara wao kurudi kwao kama pigo.





