Jonathan Sowah, mshambuliaji wa Simba SC, amezua mjadala baada ya bao lake dhidi ya JKT Tanzania kutajwa kuwa lina utata, ikidaiwa huenda alikuwa ameotea wakati akifunga.
Bao hilo lilifungwa Novemba 8, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, mchezo ambao uliisha kwa JKT Tanzania 1-2 Simba SC.
Katika mchezo huo uliojaa ushindani, JKT Tanzania walitangulia kupata bao kupitia Edward Songo, kabla ya Simba SC kusawazisha na kuongeza kupitia mabao ya Wilson Nangu aliyefunga kwa kichwa, na Jonathan Sowah aliyepachika bao baada ya kupokea pasi kutoka kwa Morice Abraham.
Akizungumzia ushindi huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC alisema wanachotambua ni kwamba walipata ushindi kwenye mchezo mgumu, kwa kutumia mbinu sahihi na silaha walizokuwa nazo ndani ya kikosi.
“Tulijua mchezo ungekuwa mgumu, ndio maana mabao yalifungwa kwa juhudi na mbinu maalum. Unaona jinsi pasi zinavyopenya katikati ya mabeki, wanaishia kujikuta wanashindwa kuchukua maamuzi haraka kwa sababu ni pasi za hatari.
“Tulitumie silaha tulizokuwa nazo, ukiwaangalia mlinda mlango Yakoub na beki Nangu, hawa ni wachezaji walioonyesha ubora mkubwa. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa pointi tatu,” alisema.




