ISMAILIA: BAADA ya timu ya JKT Queens FC kutoa sare ya pili mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, hatua ya makundi, Ismailia nchini Misri, kocha wa timu hiyo Kessy Abdallah, amewaomba mashabiki wa timu hiyo wawe na amani.
Amesema wamebakiza matumaini ya mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe , wanaandaa mpango mkakati kuhakikisha timu inakwenda hatua ya nusu fainali.
JKT Queens FC yenye alama mbili, katika mchezo wa awali, hatua ya makundi ilitoka sare tasa dhidi ya Gaborone United ya Botswana, kisha ikatoka sare ya magoli 1-1 na Asec Mimosa ya Ivory Coast, hivyo ili kusonga mbele hatua ya nusu fainali, inatakiwa kushinda mchezo ujao wa mwisho.
Kundi B, lenye timu za Asec Mimosa (Ivory Coast), Gaborone United (Botswana), TP Mazembe (DR Congo) na JKT Queens (Tanzania), kila timu inayo nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali endapo itashinda mchezo wake wa mwisho.
Gaborone United mwenye alama moja, atacheza mchezo wake wa mwisho, hatua ya makundi dhidi ya Asec Mimosa mwenye alama nne, akishinda mchezo huo, anafikisha alama nne sawa na Asec Mimosas, kwa hiyo, Gaborone United atakuwa mbele ya Asec Mimosa kimsimamo kwani, timu zikilingana alama kinachoangaliwa awali, ni matokeo ya mchezo wao, hivyo atakuwa amefuzu bila kujali matokeo ya JKT Queens FC dhidi ya TP Mazembe.
Wakati Asec Mimosas akifungwa na Gaborone, ataweza kufuzu hatua ya nusu fainali endapo, TP Mazembe yenye alama tatu, itatoka sare na JKT Queens FC yenye alama mbili, TP Mazembe pia atakuwa na alama nne, lakini atakuwa nyuma ya Asec Mimosas kwakuwa katika mchezo wao, Asec Mimosas alishinda.
JKT Queens FC akishinda mchezo wake dhidi ya TP Mazembe, atafikisha alama tano, timu yenye uwezo wa kupata zaidi ya alama hizo ni Asec Mimosas pekee, yenye alama nne, endapo itamfunga Gaborone United, itafikisha alama saba, hivyo JKT Queens FC na Asec Mimosas zitakuwa zimefuzu hatua ya nusu fainali kutoka kundi B.
Michezo ya mwisho ya makundi, itachezwa muda mmoja, saa 12:00 jioni (Misri), saa 1:00 jioni (Tanzania), ili kuepusha upangaji wa matokeo, JKT Queens FC dhidi ya TP Mazembe watanyukana katika uwanja wa Suez Canal (Ismailia), wakati huo Asec Mimosas na Gaborone United, wakichuana katika uwanja wa Right to Dream (Cairo).
The post Kocha JKT Queens awatuliza mashabiki first appeared on SpotiLEO.




