Timu Tatu za Tanzania Zashindwa Kung’ara Katika Michezo ya Kwanza ya Makundi CAF
Simba inayoiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na Azam FC na Singida Black Stars wanaopeperusha bendera ya nchi katika Kombe la Shirikisho, zimeanza kampeni zao za hatua ya makundi kwa vichapo vinavyozua maswali mapya kuhusu maandalizi na mwelekeo wa safari ya kimataifa ya klabu za Tanzania.
Matokeo hayo yametokea wakati Yanga pekee ikipata ushindi mwembamba nyumbani, huku tatu nyingine zikiambulia hasara ambazo zimeanza kutengeneza presha ya mapema katika mbio za kutafuta nafasi ya robo fainali.
Yanga Yapata Nafuu, Lakini Kazi Bado Ni Nzito
Yanga ilianza vyema kampeni za Ligi ya Mabingwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat katika Uwanja wa New Amaan, Unguja, bao likifungwa na Prince Dube.
Ushindi huo uliionyesha Yanga namna gani imeimarika kimbinu, hasa baada ya matarajio kuonesha kuwa mchezo huo ungekuwa mgumu kutokana na ubora wa Waarabu wa Morocco. Hata hivyo, ushindi huo wa mwanzo hauimaanishi kuwa safari imekuwa rahisi.
Kundi la Yanga linaendelea kuwa moja kati ya magumu zaidi likiwa na vigogo kama Al Ahly na JS Kabylie, jambo linaloifanya safari ya hatua ya makundi kuwa na ushindani mkali. Yanga sasa inaelekeza macho kwa safari ya Algeria ambako itamenyana na JS Kabylie Novemba 28 kwenye Uwanja wa Hocine Ait Ahmed, mchezo ambao unahitaji nidhamu ya hali ya juu, matumizi mazuri ya nafasi na kuepuka kuruhusu bao la mapema.
Simba Yapoteza Mchezo wa Kwanza Nyumbani
Simba SC ilipata matokeo yasiyotarajiwa baada ya kufungwa 1-0 na Petro de Luanda ya Angola kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kipigo hicho kimevunja rekodi yao nzuri ya kutopoteza nyumbani tangu Februari 2023 walipofungwa 3-0 na Raja Casablanca, na kimefanya iwe mechi ya nne mfululizo kuwashuhudia Wekundu wa Msimbazi wakikosa ushindi katika ardhi ya nyumbani.
Katika mchezo huo, Simba ilikabiliwa na changamoto mbili kubwa: kushindwa kutumia nafasi walizozitengeneza na maamuzi ya benchi la ufundi. Kocha Dimitar Pantev amekosolewa kwa kuanza mchezo bila mshambuliaji halisi kwa zaidi ya dakika 50, hali iliyowafanya washambuliaji wake kuchelewa kuingia kwenye mchezo.
Licha ya kipigo hicho, nafasi ya kufuzu robo fainali bado ipo, hasa ikizingatiwa kwamba Simba imewahi kupoteza mechi mbili katika hatua kama hii na bado ikapenya. Hata hivyo, mashabiki wanataraji mabadiliko ya kimkakati kuelekea mchezo ujao dhidi ya Stade Malien ambao waliilazimisha sare Esperance ya Tunisia.
Azam FC Yaangukia Kichapo Kizito Katika Debut ya Makundi CAF
Azam FC, ikiwa katika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia yake, ilianza vibaya baada ya kuchapwa 2-0 na Union Maniema ya DR Congo. Matokeo hayo yameibua mjadala kuhusu utulivu wa kikosi hicho, hasa ikizingatiwa kuwa ilikuwa mechi yao ya kwanza katika hatua ya juu kabisa ya mashindano ya CAF.
Changamoto kubwa kwa Azam ilikuwa kwenye safu ya ushambuliaji, ambapo Japheth Kitambala alikosa nafasi muhimu—ikiwemo mabao mawili ya wazi—zikiwa ni dhidi ya timu yake ya zamani. Makosa hayo ya ufungaji, pamoja na mapungufu ya ulinzi ambayo yaliwaruhusu wenyeji kupata mabao mawili, yameifanya Azam kurudi kwenye meza ya tathmini.
Azam inarejea nyumbani kujiandaa na Wydad Athletic ya Morocco Novemba 28, timu ambayo ilianza kampeni yake kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nairobi City Stars. Ili kuepuka matatizo zaidi, Azam italazimika kuimarisha safu ya ulinzi na kuongeza makali ya washambuliaji wake ili kutumia vizuri faida ya uwanja wa nyumbani.
Singida Black Stars Yapoteza Lakini Yaonesha Mng’aro wa Kimbinu
Singida Black Stars, ambayo inashiriki hatua ya makundi kwa mara ya kwanza, ilipoteza 2-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria inayoongozwa na kocha Sead Ramovic, aliyewahi kunukia kwenye benchi la Yanga. Ingawa walipoteza, Singida ilionesha mpira wa kueleweka, kupambana na kutengeneza nafasi, jambo linaloonyesha uwepo wa msingi mzuri wa kujenga matokeo katika mechi zijazo.
Timu hiyo sasa inajiandaa kukabiliana na Stellenbosch ya Afrika Kusini katika Uwanja wa New Amaan mnamo Novemba 30, ikiwa na motisha ya kupata pointi muhimu kabla ya mechi mbili mfululizo dhidi ya AS Otoho mwakani. Habari njema kwa Singida ni kurejea kwa kiungo mkongwe Khalid Aucho, ambaye anakadiriwa kuongeza uthabiti na uzoefu kwenye eneo la kati.




