SIMBA huenda wakapata fursa ya kumpata Kocha Miguel Gamondi baada ya uongozi wa Singida Black Stars kuweka wazi kuwa uko tayari kufuata taratibu za kimkataba endapo kutakuwa na maombi rasmi kutoka klabu yoyote inayomhitaji kocha huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba wako kwenye mipango ya kumchukua Gamondi ili awe kocha mkuu wa timu hiyo, ambapo inatarajiwa ajiunge na wekundu hao baada ya kumalizika kwa michuano ya AFCON ijayo.
Hata hivyo, Meneja Rasilimali Watu wa Singida Black Stars, Muhibu Kanu amesema hadi sasa hawajapokea maombi yoyote rasmi kutoka klabu yoyote inayomhitaji Gamondi wala mchezaji yeyote kutoka ndani ya kikosi chao.
Kanu amesisitiza kuwa Singida Black Stars haijawahi kuwa kikwazo kwa mtu yeyote anayehitaji kuondoka ndani ya klabu hiyo, mradi tu ahakikishe anafuata taratibu zilizowekwa kisheria na kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.
Amesema endapo kocha ataona kuna maslahi makubwa sehemu nyingine, uongozi utakaa mezani kuangalia mkataba wake unasemaje kabla ya kuchukua hatua, akisisitiza kuwa mikataba ipo na kinachozingatiwa zaidi ni kufuata sheria.
“Singida Black Stars hatutakiwi kuwa kikwazo kwa mtu kwenda kupata maslahi makubwa. Umeona Gamondi alipotakiwa kusaidia timu ya Taifa tulimruhusu, hivyo kama kuna klabu inamhitaji, ije mezani tufuate taratibu,” amesema Kanu.
The post SINGIDA BLACK STARS YAIPA MWANYA SIMBA SC appeared first on Soka La Bongo.








