MILAN: RAIS wa Serie A Ezio Simonelli amethibitisha kuwa mechi ya Serie A kati ya AC Milan na Como iliyopangwa kuchezwa mjini Perth nchini Australia, mwezi Februari mwakani itaendelea kama ilivyopangwa.
Kauli hiyo inakuja baada ya ripoti za vyombo vya habari vya Italia wiki iliyopita kudai kuwa mchezo huo ulikuwa hatarini kuahirishwa, kufuatia wasiwasi wa Serie A juu ya masharti waliyoyataja kuwa hayakubaliki kutoka kwa Shirikisho la Soka la Asia (AFC). Simonelli mwenyewe alisema wakati huo kuwa mchakato ulikuwa bado unaendelea.
Simonelli sasa amesema changamoto hizo zimetatuliwa, hasa suala la uteuzi wa waamuzi, baada ya mazungumzo na aliyekuwa refa nguli wa Italia na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA, Pierluigi Collina.

“Tulikuwa na mashaka kadhaa kuhusu baadhi ya masharti yaliyowekwa, ambayo tuliona hayatekelezeki, kama vile kuombwa kutumia waamuzi wa Shirikisho la Asia, ilhali tuna imani kubwa na waamuzi wetu wa Italia,” – Simonelli ameliambia shirika la habari la Mediaset.
“Collina alituhakikishia juu ya ubora wa waamuzi wa Asia, na hata akataja baadhi ya waamuzi wanaoweza kupewa mchezo huo. Hilo ndilo lilikuwa kikwazo kikubwa zaidi, lakini tumekivuka kutokana na hakikisho lake,” – aliongeza.

Shirikisho la Soka Italia (FIGC) liliidhinisha ombi la Serie A kuhamisha mchezo huo uliopangwa Februari 8, baada ya Uwanja wa San Siro kutopatikana kutokana na kuandaliwa kwa sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Milano-Cortina.
Mwezi Oktoba, UEFA ilitoa idhini kwa kusita kwa mchezo huo wa Serie A, uamuzi uliokwenda sambamba na mpango wa LaLiga kuchezesha mechi kati ya Barcelona na Villarreal mjini Miami, mpango ambao baadaye ulifutwa kufuatia upinzani mkali wa ndani.
The post Kimeeleweka, Milan V Como kupigwa Australia first appeared on SpotiLEO.








