RAIS wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu Afrika (ACA), Hersi Said, ameweka wazi kuwa kujiunga na umoja huo si jambo la lazima bali ni hiari ya kila klabu kulingana na maslahi yake.
Kauli hiyo inaonesha kuwa msimamo wa Klabu ya Simba wa kutaka kufahamu faida na malengo ya kuanzishwa kwa ACA ni wa msingi, kwani kila klabu ina haki ya kujiridhisha kabla ya kufanya maamuzi ya kujiunga na umoja wowote.
Hersi amesema ACA imeanzishwa kwa lengo la kuimarisha umoja wa vilabu barani Afrika na kuleta mwelekeo mpya wa maendeleo ya soka, akifafanua kuwa hata barani Ulaya, umoja kama huo ulianzishwa miaka 18 iliyopita na ulianza kwa vilabu 14 pekee.
Ameeleza kuwa kutokana na kuwa ni suala la hiari, mara tu faida zake zitakapoonekana wazi, vilabu vingi vitaanza kujiunga kwa wingi. Kwa sasa, amesema vilabu 10 tayari vimesajiliwa, huku vingine 32 vikiwa kwenye mchakato wa usajili ambao ukikamilika vitatangazwa rasmi.
Hersi ameongeza kuwa baadhi ya vilabu vinamilikiwa na jamii, hivyo hulazimika kupitia mchakato wa vikao na makubaliano ya pamoja kabla ya kufanya uamuzi, wakati vilabu vya mtu binafsi navyo huhitaji mashauriano ya ndani kabla ya kujiunga.
Amesisitiza kuwa si sahihi kusema vilabu vinasuasua, bali ni muhimu kila klabu kuelewa faida itakayopata. Amefafanua kuwa ndani ya ACA kuna wajumbe 12, kila kanda ikiwa na mjumbe wake ambaye jukumu lake ni kuelimisha na kueleza vilabu juu ya manufaa ya kujiunga na umoja huo.
The post KUJIUNGA ACA NI HIARI, HERSI AFUNGUKA HAYA appeared first on Soka La Bongo.





