Jumla ya shilingi bilioni 866.47 zimetumika katika kuboresha utoaji wa huduma za Afya Msingi nchini katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa Octoba 1,2024 na Naibu Waziri ( Afya) Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Festo Dugange katika ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Afya nchini unaofanyika Zanzibar katika Mji wa Fumba.
Mhe. Dugange amesema kuwa matokeo ya uwekezaji huo mkubwa umeleta mabadiliko makubwa katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma pamoja na utoalewaji wa huduma bora za afya ya Msingi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Ameeleza kuwa hadi kufikia Septemba mwaka 2024, Sekta ya afya ngazi ya msingi hapa nchini ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 7,136 zikiwemo Zahanati 6,058 Vituo vya afya 896, Hospitali za Halmashauri 177, Hospitali zenye hadhi ya Wilaya 5. Takwimu hizi zinaonyesha ongezeko kubwa la idadi ya vituo katika Afya ya msingi ikilinganishwa na idadi ya Vituo 5,270 mwaka 2015.
Kupitia mafanikio hayo kwa mwaka, 2023, wateja milioni 26.9 sawa na 78% ya wagonjwa wote nchini, walipata huduma katika Vituo vya afya ya Msingi kama wagonjwa wa nje yaani (OPD), wateja 854,318 sawa na asilimia 65% walipata huduma ya kulazwa (IPD)” Amebainisha
Ameeleza kuwa mifumo ya utoaji wa huduma ya Afya ya msingi imeimarika ambapo vifo vya akina mama wajawazito vimepungua kutoka 556/100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104/100,000 mwaka 2022.
“Katika eneo la mama na mtoto jumla ya wateja milioni 1.6 sawa na asilimia 91% ya wajawazito wote nchini walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi na waliokuwa na uzazi pingamizi wakafanyiwa upasuaji walikuwa ni 125,318” Amebainisha Mhe. Dugange