Na Farida Mangube
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewataka Wataalamu wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuhimiza utekelezaji wa utunzaji na uendelezaji wa misitu nchini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
Amebainisha hayo katika siku ya kufunga Maadhimisho ya Miaka 50 ya kuanzishwa kwa Kitivo cha Mafunzo ya Misitu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambapo amesema kitu wanachotakiwa kukifanya ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuisadia kupata uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa Misitu katika maeneo yote kwa ajili ya kukiwezesha kizazi kijacho kuja kunufaika na misitu na mazingira kiujumla.
Aidha Malima amesema Wataalamu kutoka SUA wanapaswa kuifahamisha jamii athari zinazotokea kutokana na uharibifu wa misitu ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na shughuli za binadamu ikiwemo kuchoma mkaa, kukata kuni na shughuli za kilimo hasa maeneo ya pembezoni mwa miji.
Kwa upande wake Bi. Metrida Kaijage Mtaalamu wa Sheria za misitu kutoka SUA amesema Wataalamu wana wajibu wa kutunga Miswada na kupeleka kwa serikali ili kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali misitu lakini pia amezitaka Taasisi kama SUA kutafuta washirika ambao watashirikiana nao katika uratibu wa uhifadhi misitu.
“Natumaini kama Wataalamu kutoka SUA mtaendelea kufanya tafiti zenye tija kuhusiana na Misitu ikiwemo njia sahihi za kutatua changamoto za kidunia ambazo zinaathiri misitu na mazao yake pamoja na tafiti za kisayansi za misitu”, amesema Bi. Metrida Kaijage.
Naye Prof. August Temu ambaye pia ni Mtaalamu wa Misitu kutoka SUA amesema anaiona Tanzania ikiendelea kufanya vizuri katika utunzaji wa Misitu kwani SUA inaendelea kuzalisha Wataalam wengi wa Misitu ambao watazidi kuwa vinara wa utunzaji Misitu na rasilimali zake kwa manufaa makubwa ya jamii na kizazi cha kesho.
“Miaka 50 ijayo anaiona Tanzania ikifikia hatua ya nchi kama Finland na China ambazo zinatumia vizuri Mazao ya Misitu kwani katika nchi hizo kila zao la Msitu lina matumizi katika viwanda vya uzalishaji malighafi, ambazo zinatumika kuinua uchumi wa nchi hivvo naamini Tanzania itafikia hatua hiyo kama endapo tu watu wataweza kutunza Misitu kikamilifu”, amesema Prof. Temu
Mhe. Diwani wa Kata ya Magadu Bw. Juma Issa Kiduka amesema, elimu inayotolewa na SUA imepunguza matukio ambayo yalikua yanahatarisha utunzaji wa misitu ikiwemo uchomaji moto katika maeneo ya milima ambayo imezungukwa na Misitu hivyo amewaomba Wataalamu kutoka Chuo hicho kuendelea kutoa elimu na kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wa kata ya Magadu ili kuendelea kupunguza hatari ambazo husababishwa na binadamu zinazoathiri Misitu.