Na WAF – KIGOMA
Madaktari Bingwa 57 wa Rais Samia wamewasili na kupokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Hassan Rugwa kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwenye Halmashauri zote za mkoa kwa muda wa siku sita.
Bw. Rugwa amewakaribisha madaktari bingwa hao leo Oktoba 7, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Thobias Andengenye CGF (RTD) ambao watatoa huduma za kibingwa za Afya na kuwajengea uwezo watoa huduma mkoani humo.
“Tunashukuru sana kwa huduma hii ya madaktari bingwa wa Rais Samia kuja mkoani kwetu na tunawakaribisha sana kwani huduma hizi ni za kibingwa watakazozitoa kwa muda wa siku sita zitahusu juu ya kuokoa maisha ya mtu na thamani yake ni kubwa haiwezi kulinganishwa na chochote ”. Amesema Bw. Rugwa
Aidha Bw. Rugwa ameipongeza na kuishukuru Wizara ya Afya na Ofisi ya Raisi Tamisemi kwa kuona ubora na umuhimu wa kuleta huduma hii ya madaktari bingwa ikiwa na Lengo la kuboresha huduma ikiwemo kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi na pia huduma jumuishi za kibingwa kwa mkoa wa Kigoma
kwa upande wake Mratibu wa huduma hizo za madaktari bingwa mkoa wa kigoma Bi. Jackline Ndanshau amesema mpango wa utoaji huduma za kibingwa ngazi ya Halmashauri kwa kutumia programu iitwayo “Madaktari bingwa wa Dkt. Samia”, ina malengo makuu matatu ambapo malengo hayo ni madhubuti na muhimu kwa wananchi
“Malengo ya programu hii ni pamoja na kusogeza huduma za kibingwa katika Halmashauri zote 184 nchi nzima , Kuimarisha na kuanzisha wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu “NCU”, na Kutoa mafunzo elekezi kazini kwa watoa huduma za afya, ili kuimarisha ubora wa huduma za afya katika hospitali walizopelekwa madaktari bingwa wa Rais Samia.” Amesema Bi. Jackline
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Bwana Damas Kayera amesema uwepo wa madaktari bingwa katika mkoa wa Kigoma ni furaha kubwa kwa wananchi wa kigoma kuweza kupata huduma kwa karibu ambapo huduma hizo za kibingwa wangeweza kuzifuata pengine katika hospitali ya Taifa muhimbili na hata baada ya kuondoka madaktari hao basi watoa huduma wataweza wamejengewa uwezo mkubwa na mzuri
“Shughuli hii inafaida kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na kupata huduma bingwa na ambazo kwa sasa zitakuwa zimesogezwa karibu nao na pia kwa watoa huduma wetu kuweza kupata ujuzi bobevu .” Amesema Bw. Damas Kayera