Na. WAF – HAI
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Hai Dkt. Emmanuel Minja amesema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kutoka kwa Madaktari bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan walioweka kambi Wilayani humo kwa siku saba.
Dkt. Minja amesema hayo leo wakati wa kambi ya Madaktari Bingwa hao wakiendelea kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali ya Wilaya ya Hai.
Dkt. Minja amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa kwani kwa siku ya jana wamepokea wagonjwa zaidi ya 90 ambao wamefuata huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari hao.
“Wananchi wamekuja maalum kwa ajili ya madaktari bingwa na leo pia tunatarajia idadi ya watu itaongezeka na kumbuka wananchi wanaotibiwa wapo wanaolipa fedha taslimu na wanaotumia bima kwahiyo hata mapato ya hospitali yataongezeka,” amesema Dkt. Minja.
Ameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa katika Hospitali ya wilaya ya Hai kwani huduma hizo zitakuwa endelevu na kuleta tija kwa wananchi wa Hai.
Aidha, Dk. Minja amesema amewapokea Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Daktari bingwa wa watoto na watoto wachanga, Daktari wa usingizi na ganzi, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Daktari bingwa wa upasuaji na mfumo wa mkojo, Daktari bingwa wa kinywa na meno na Muuguzi bingwa.
“Kazi imeanza kwa kweli namshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hii ya kufungamanisha huduma za kibingwa na wananchi wa ngazi ya msingi lakini kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya walipo hapa kituoni kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi na kupunguza rufaa,” amemshukuru Dkt. Minja.
Amesema kuwa kutokana na hamasa iliyofanyika katika Wilaya hiyo wananchi wengi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa na bingwa bobezi na kuleta tija ya uwepo wa kampeni hii ya kufungamanisha Huduma zakibingwa na bingwa bobezi na wananchi wa ngazi ya msingi.
“Madaktari hawa bingwa wanatibu huku wanafundisha yaani mafunzo yanaendelea lakini hapo hapo matibabu yanaendelea hivyo sisi watu wa Hai tumenufaika sana na ujio wa hawa Madakatari bingwa na kufanya wananchi wengi kupata huduma hizi Wilayani hapa,” ameeleza Dkt. Minja.
Amesema menejimenti ya hospitali inahakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwezesha vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana kwa wakati ili kuleta tija ya Huduma hizo za kibingwa kupatikana katika ngazi ya msingi.
“Pia tuliandaa timu ya madaktari ambao watakuja kuungana na hawa madaktari bingwa ili kuongeza ujuzi na kusaidia huduma za kibingwa kupatikana katika hospitali yetu kipindi watakapo kuwa wamehitimisha kambi hiyo,” ameongeza.
Kwa upande wake mmoja wa wananchi waliofika Hospitalini hapo kupata Huduma hizo Isaya Mushi (68) ameishukru serikali chini ya uongozi imara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi wake na kuwasogezea Huduma za kibingwa karibu yao.
“Umati huu ni ishara tosha kuwa wananchi tunauhitaji wa Huduma hizi za kibingwa katika maeneo yetu ndo maana tumejitokeza kwa wingi kiasi hiki,” amebainisha Isaya.