WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, leo, tarehe 3 Oktoba 2024 ametembelea na kukagua Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo, wilayani Ludewa.
Akiwa chuoni hapo, Prof. Mkenda ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa juhudi zake za kuboresha elimu ya ufundi stadi nchini, huku akiagiza mamlaka hiyo iangalie kwa makini mahitaji ya ujuzi katika jamii ya Ludewa na Njombe kwa ujumla, akitolea mfano mradi wa uchimbaji na uchakataji wa chuma uliopangwa kufanyika katika eneo la Liganga, pamoja na shughuli za kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
Aidha, Prof. Mkenda amewaomba wananchi wa Njombe kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kutokana na jitihada zake za kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata mafunzo ya ujuzi ili kuwawezesha kuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi.
“Kwa Rais ambaye anafanya kazi nzuri kama hii, ni muhimu kumuunga mkono. Tusipojifunza kusemea mazuri ambayo yanafanywa, watakuja watu ambao watasema mabaya na kufanya ionekane kazi haifanyiki,” ameongeza.
Akizungumzia shughuli za chuo hicho, Waziri Mkenda ameonesha matumaini kuwa chuo cha VETA Mkoa wa Njombe kitakuwa kiungo muhimu katika kuwaandaa vijana wa mkoa wa Njombe na maeneo jirani kwa ajili ya fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kutokana na miradi mikubwa inayokuja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, ameongeza ushauri wake kuhusu maeneo ya kipaumbele katika mafunzo ya ufundi yanayopaswa kutolewa chuoni hapo akisema ni muhimu kuzingatia mafunzo yanayohusiana na ujuzi unaohitajika kwenye miradi ya madini, hasa kwa kuzingatia uwepo wa miradi mikubwa ya uchimbaji inayotarajiwa kuanza katika eneo la Liganga.
Aidha, Thomas ameshauri mafunzo yahusishe pia utengenezaji wa vifaa vya uvuvi na ufugaji wa samaki, ikiwemo vizimba, kwa kuwa wananchi wengi wa Ludewa na maeneo ya jirani wanazungukwa na Ziwa Nyasa.
“Ni muhimu kuhakikisha vijana wanapata mafunzo ambayo yatawawezesha kuzitumia ipasavyo fursa hizi za asili zilizopo katika maeneo yetu,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Naye Mbunge wa Ludewa, Mheshimiwa Joseph Kamonga, alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri, ameeleza kuwa tayari amekubaliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kuwa eneo linalozunguka Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe lipangwe rasmi ki-mji na kupimwa, hatua ambayo amesema imelenga kuleta maendeleo katika mazingira ya chuo hicho kwa kuboresha miundombinu na fursa za kiuchumi kwa jamii ya inayozunguka chuo.
Mbunge Kamonga pia ametoa ombi maalum kwa Waziri Mkenda kusaidia ukamilishaji wa kituo cha afya ambacho ujenzi wake ulianza kwa nguvu za wananchi, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi, walimu, na jamii inayozunguka chuo hicho.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omary, amezungumzia umuhimu wa kupanua mafunzo ya ufundi wa umeme katika chuo hicho na maeneo mengine ya mkoa, akibainisha kuwa Njombe ina wazalishaji wengi wa umeme, jambo ambalo linatoa fursa kubwa kwa vijana kujifunza kwa vitendo na kuendeleza ujuzi huo.
Omary amesisitiza kuwa ni muhimu kushirikiana na wazalishaji wa umeme ili kuhakikisha vijana wanapata mafunzo ya kiufundi yanayowezesha kukidhi mahitaji ya soko na kuwezesha kurithisha ujuzi wa asili kutoka kwa wazee wa mkoa huo, ambao wamekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika kazi za uzalishaji umeme.
“Hili litasaidia si tu katika kuendeleza maarifa, bali pia kutunza urithi wa kiufundi kwa vizazi vijavyo,” alisema Judica Omary.
Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe unatekelezwa na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Njombe na umefikia asilimia 95 ambapo baadhi ya miundombinu ya chuo imeruhusu mafunzo kuanza kutolewa.
Akitoa taarifa kuhusu kuanza kwa Mafunzo chuoni hapo, Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe, Wilfred Mwatulo amesema chuo kilianza na Mafunzo ya muda mfupi ambapo vijana 14 wamehitimu katika fani za Matumizi ya Kompyuta; Utengenezaji Kompyuta na Umeme wa Majumbani.
Amesema, Julai mwaka huu (2024) walidahili wanafunzi 22 wa ngazi ya tatu katika fani ya Umeme na kwamba mwaka 2025 wamepanga kudahili wanafunzi 200 wa ngazi ya kwanza katika fani za Uashi, Ufundi Bomba, Umeme wa Majumbani, TEHAMA na Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya nguo.