Wananchi wa vijiji pembezoni mwa Bwawa la Mkomazi hatimae kuona ndoto ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kutaka kujenga bwawa hilo la umwagiliaji sasa kutimizwa na Rais Dkt. Samia.
Ameeleza hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) mbele ya wananchi hao tarehe 5 Oktoba 2024 wakati wa mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mangamtindiro, Kata ya Mkomazi, mkoani Tanga.
“Kati ya mabwawa 14 yanayojengwa mwaka 2024/25 ni Bwawa hili la Mkomazi lenye gharama ya shilingi bilioni 18 na litanufaisha wananchi zaidi ya 20,000; Kata zaidi ya 7 na vijiji zaidi ya 28. Nawashukuru sana wakazi wa Goha waliotoa ekari 10 kupisha mradi huu wa kihistoria,” amesema Waziri Bashe.
Ameeleza kuwa mradi huo pia utahuisha ujenzi wa mabomba mawili yenye urefu wa kilometa 16 na 29 ambayo yatakuwa yanasafirisha maji pande tofauti, Pamoja na Ujenzi wa mifereji mikuu, mifereji ya matupio, ujenzi wa ghala, Kituo cha zana za kilimo, mashine ya kukoboa mpunga na barabara za mashamba na za kusafirishia mavuno.
Aidha, Waziri Bashe pia ameongea na wakazi wa Kata za Chekelei, Magila Gereza, Mazinde, Momba na Makuyuni ambao ni wanufaika wa bonde la Mkomazi ambapo watajengewa miundombinu ya umwagiliaji na kufanya mradi wote pamoja na Bwawa la Mkomazi kuwa na thamani zaidi ya shilingi bilioni 100. Miradi hiyo misogo pia itakuwa na huduma kama za Bwawa la Mkomazi kama vile maghala, vituo vya zana za kilimo, n.k.
Waziri Bashe pia ameielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa kuhakikisha Wafuasi wanatengewa eneo la kunywesha mifugo, huku Bwawa la Mkomazi likizungushiwa fensi ya umeme kulinda miundombinu yake, na kuweka taa za barabarani za solar.