KAMANDA wa kikosi 834 KJ Makutopora Kanali Festo Mbanga amewahamasisha Watanzania kuwapeleka watoto kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili wapate mafunzo yatakayowajengea Upendo,uzalendo, ujasiriamali na ukakamavu.
Kanali Mbanga ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na kikundi cha OPERESHENI KAMBARAGE kilichopitia mafunzo katika kikosi hicho mwaka 1990 hadi 1991 baada ya kutembelea kambini hapo na kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti.
“Watanzania hamasisheni kupeleka watoto kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ili waweze kupatiwa mafunzo yatakayowajengea Upendo,uzalendo, ujasiriamali na ukakamavu ili waweze, kukabiliana na changamoto za maisha,”amesema
Aidha ameongeza kuwa ujio wa kikundi hicho imekuwa chachu kwao jambo ambalo linaonesha kuwa wapo baadhi ya watu waliopitia mafunzo ya JKT na kuna mahali yamewasaidia katika maisha yao.
Kwa upande Bw. Vivian Komu mmoja wa Viongozi wa kikundi cha OP- KAMBARAGE amesema kuwa lengo la kutembelea Kikosi hicho ni kuyaenzi mafunzo waliyoyapata miaka 33 iliyopita ambayo yamewasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uzalendo kwa maendeleo ya Taifa.
“mafunzo tuliyoyapata mwaka 1990 mpaka 1991 hapa Makutopora yametufaa Sana katika maisha yetu na taifa kwa ujumla kwani mpaka leo tunakutana hapa kila mmoja anamajukumu yake na ukweli ni kwamba nidhamu, uzalendo na ukakamavu wetu ni matokeo ya kupitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, “amesema Komu
Naye Frida Marco amesema Taifa lipo salama kwa sababu ya kuwa na vijana wengi wanaopitia Jeshini, hivyo wazazi wasiwafiche watoto pindi wanapotakiwa kujiunga na Jeshi.
” Wazazi waacheni watoto wajiunge na JKT kwa maslahi ya Taifa kwani mtoto akipata mafunzo ya Jeshi huwezi kusikia anajiunga na vikundi viovu, migomo ama maandamano yasiyokuwa na maana,kazi yake popote atakapokuwepo atakuwa anaweka maslahi ya Taifa mbele kutokana na Uzalendo na nidhamu aliyefundishwa kutoka Jeshini, ” ameeleza Frida
Kikundi cha OPERESHENI KAMBARAGE ni vijana waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 1990 hadi 1991 MAKUTOPORA.