Mhadhiri, wa Chuo hicho na Daktari Bingwa wa watoto Profesa Karim Manji (katikati) akipokea zawadi ya picha wakati wa hafla ya kumpongeza na kutambua mchango wake katika Chuo hicho na Tanzania kwa ujumla baada ya kushinda tuzo ya juu ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard Marekani (Havard T.H.Chan School of Public Health) aliyopokea hivi karibuni na kuifanya MUHAS kuwa chuo cha tatu kwa ubora Afrika.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (Kushoto) akiangalia moja ya tuzo za Mhadhiri, wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Daktari Bingwa wa watoto Profesa Karim Manji (kulia) Wakati wa hafla ya kumpongeza na kutambua mchango wake katika Chuo hicho na Tanzania kwa ujumla baada ya kushinda tuzo ya juu ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard Marekani (Havard T.H.Chan School of Public Health) aliyopokea hivi karibuni na kuifanya MUHAS kuwa chuo cha tatu kwa ubora Afrika. Hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 15,2024 katika ukumbi wa Chipe chuoni hapo ǰijini Dar es Salaam.
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SERIKALI imesema itataendelea kuwekeza katika sayansi, teknolojia, tafiti na elimu tiba ili kuongeza rasilimali watu watakaozingatia utu na ubinadamu katika utoaji wa huduma.
Pia watafiti wa kisayansi wanapaswa kuthaminiwa kwani uwepo wao unawezesha msukumo wa masuala mengi ikiwemo afya.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema hayo leo Oktoba 15,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumpongeza na kutambua mchango wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Daktari Bingwa wa watoto, Profesa Karim Manji.
Profesa Manji ni mshindi wa tuzo ya juu ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard Marekani (Havard T.H.Chan School of Public Health) aliyopokea hivi karibuni
Profesa Mkenda amesema kuwa imekuwa utamaduni uliozoeleka nchini kwa kuwatambua wanasiasa, wanamichezo na wanamuziki hivyo, ni wakati wa kuwatambua maprofesa na wanasayansi ambao wamechangia mabadiliko mbalimbali nchini.
Amesema miongozo mbalimbali ya utoaji huduma kwa watoto imechangiwa na tafiti alizofanya Profesa Manji hivyo kuwezesha kuokoa maisha ya watoto wengi hususan watoto njiti.
“Tukitaka kusogea tuhakikishe tunawatambua watu wanaookoa maisha ya watu kwa kufanya gunduzi na tafiti nyingi. Tanzania inajivunia Profesa Manji umetuheshimisha na tunaomba wengine mnaoendelea kufundisha, muongeze kasi na bidii katika tafiti,” amesema Profesa Mkenda.
Ameongeza kuwa ili kupata wanasayansi bora lazima washindane na watafiti wengine duniani kwa kuchapisha tafiti zao kwenye majarida ya kimataifa hivyo kuiweka Tanzania kwenye ramani nzuri ya ukuaji wa sayansi.
Aidha Profesa Mkenda amewataka watafiti na wanasayansi kutojifungia badala yake wafanye tafiti zenye kutatua changamoto katika jamii, kuokoa maisha na kuboresha utoaji wa huduma.
“Tutaongeza uwekezaji katika sayansi na teknolojia, uhandisi na elimu tiba tupate rasilimali ya kutosha katika eneo hili ambalo bado hatujafanya vizuri. Samia Scholarship na nyingine kwa ajili ya wakufunzi zitaongezeka,” alieleza Profesa Manji.
Kwa upande wake, Profesa Manji amesema kuwa anajisikia fahari kuthaminiwa na serikali pamoja na chuo hicho na kueleza kwamba wapo wengi ambao wamechangia katika kuboresha sekta ya afya na huduma kwa ujumla nchini.
Ameeleza kuwa pamoja na elimu yake kuwa na changamoto mbalimbali, amefundishwa ubinadamu na utu katika kutoa huduma jambo ambalo watu ‘wengi wamekuwa wakimshangaa kwa kujichanganya na watu wa chini.
“Watu wananishangaa kukaa na watu ambao hawaendani na mimi, sioni shida kukaa nao na kuwapa elimu ya lishe au kuondoa unyanyapaa dhidi ya magonjwa mbalimbali. Kubeba matikiti mabegani na kujiona tofauti kwa sababu wewe ni Profesa au kiongozi, si sawa tunatakiwa kujishusha kuwafikia walengwa,” ameeleza
Amesema anaona fahari anapoona mama mwenye watoto mahututi anatabasamu kwamba anashukuru Mungu hata kwa maumivu anayopitia.
“Dunia inabadilika lakini hatupaswi kubadilika kiroho na kibinadamu, tuwashike watu na kuwapa faraja, si lazima wawe na fedha itasaidia wengi,” amesema.
Ameongeza kuwa “Mambo niliyofanya kwa Tanzania nikaacha legacy, sasa naweza kufa kwa amani, nikiwa nimefumba macho yangu…kama unaweza kuokoa maisha ya watoto wanaoharisha kwa kuwapatia ORS na Zinc, hayo ni mafanikio makubwa.”
Amesema kuwa hata atakapostaafu, hatamani kwenda nchi nyingine zaidi ya Tanzania kama wazazi wake walivyolazwa katika ardhi hiyo.
Naye, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa akizungumzia mafanikio ya Prof. Manji amesema mtaifiti huyo ni mfano wa kuigwa, hazina kwa taifa na mtafiti mkubwa Muhas ingependa kuendelea naye.
Prof Kamuhambwa amesema mafanikio ya Muhas kuwa chuo cha tatu kinachoongoza kwa kufundisha, tafiti, huduma Kusini mwa Jangwa la Sahara pia yamechangiwa uwepo wa Prof Manji kwenye utekelezaji wa tafiti mbalimbali hivyo wataendelea kufundisha, kutafiti na kutoa huduma za afya nchini.
“Juni 2023 jarida la Time Higher Education liliitaja MUHAS kama chuo Kikuu cha tatu kwa ubora Afrika, ubora wa elimu yetu unatokana na tafiti na huduma tunazozitoa,” amesisitiza.
Amesema wataalamu wa afya ambao wamefanya kazi nzuri nchini, wanatakiwa kuenziwa na kutunzwa kwani wamechangia mabadiliko ya sekta ya afya na mapendekezo waliyotoa yameweza kutumiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Bado tunahitaji wakufunzi ambao watawasaidia wafanyakazi wetu kuwa na utu na ubinadamu wanapotoa huduma kwani wapo wenye midomo michafu na maneno mabaya na hawajali,”
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (kulia) akiteta jambo na Makamu Mkuu wa chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Apolinary Kamuhabwa wakati wa hafla ya kumpongeza na utambua mchango wa Mhadhiri, wa Chuo hicho na Daktari Bingwa wa watoto Profesa Karim Manji baada ya kushinda tuzo ya juu ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard Marekani (Havard T.H.Chan School of Public Health) aliyopokea hivi karibuni na kuifanya MUHAS kuwa chuo cha tatu kwa ubora Afrika.
Mhadhiri, wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Daktari Bingwa wa watoto Profesa Karim Manji akiongea kwa furaha kuelezea safari yake ya maisha wakati wa hafla ya kumpongeza na kutambua mchango wake katika Chuo hicho na Tanzania kwa ujumla baada ya kushinda tuzo ya juu ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard Marekani (Havard T.H.Chan School of Public Health) aliyopokea hivi karibuni na kuifanya MUHAS kuwa chuo cha tatu kwa ubora Afrika.