Na Farida Mangube
Wafugaji wametakiwa kubadili mtazamo wa ufugaji wa mazoea na badala yake kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ya mifugo ili kuongeza uzalishaji wenye tija na kudhibiti magonjwa kwa ufanisi zaidi.
Rai hiyo imetolewa na Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Esron Karimuribo, wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo na vyeti kwa wanafunzi waliohitimu na kufanya vizuri katika masomo yao.
Profesa Karimuribo amesema kuwa hakuna tija kwa wafugaji wanaoendelea kufuga kienyeji bila kufuata tiba na ushauri wa kitaalamu. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wafugaji kutumia mbinu za kisasa za ufugaji ambazo zinalenga kuongeza uzalishaji na kudhibiti magonjwa ya mifugo. Pia amewataka wahitimu wa SUA kutumia elimu waliyoipata kuwasaidia wafugaji kuboresha mbinu zao za ufugaji.
“Ndugu zangu, wafugaji hawawezi kufikia tija ya kweli ikiwa wataendelea kufuga kienyeji na kutumia tiba zisizo na uhakika. Ninyi kama wahitimu, mnapaswa kwenda kuwapa msaada unaotokana na maarifa mliyoyapata chuoni hapa,” amesema Profesa Karimuribo.
Aidha, amewataka wahitimu hao kutumia vizuri taaluma zao ili kuweza kujiajiri na kuwajiri wengine, na kuondoa dhana ya kutegemea ajira peke yake. “Vijana wengi wanaomaliza masomo hukimbilia kutafuta ajira, badala ya kutengeneza fursa za kuajiriwa na kuajiri wengine. Taaluma mliyoipata inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutengeneza ajira,” aliongeza Profesa Karimuribo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Masomo ya Shahada za Awali SUA, Dkt. Hamza Tindwa, amewahimiza wafugaji kutumia wataalamu waliobobea kutoka SUA, akisisitiza kuwa chuo hicho ndicho kinachoongoza kwa kutoa wataalamu wenye weledi katika fani za afya ya mifugo na kilimo.
Mmoja wa wanafunzi waliopewa tuzo ya kufanya vizuri katika masomo, Zainabu Yasini, ameishukuru SUA kwa kuwapatia elimu bora itakayowasaidia kufanikisha maisha yao na kuchangia kwa ufanisi katika sekta ya ufugaji. Amewataka vijana wenzake kuwekeza zaidi katika taaluma zao na kuchangia kwa vitendo maendeleo ya sekta hiyo.