Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amezindua jengo la utawala katika Shule ya Sekondari ya Mwandege lililojengwa na kukamilika kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga lililogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 119.9.
Bashungwa amezindua jengo hilo leo Oktoba 23, 2024 Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani ikiwa ni muendelezo wa ziara yake maalum katika Mkoa huo ya kukagua utekelezaji na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo kwenye Sekta mbalimbali katika Mkoa wa Pwani na ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa kazi nzuri ya usimamizi wa fedha hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa amezindua daraja katika barabara ya Mwanambaya – Mipeko eneo la bonde la mto Mzinga lililojengwa na kusimamiwa na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara na kuwezesha mawasiliano katika Kata ya Mipeko, Mwanambaya na Mbande ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii kwa Wilaya za Mkuranga na Temeke.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kumtafuta Mkandarasi kwa ajili ya kujenga daraja la kisasa la Mto Mzinga ili kusaidia kupunguza foleni katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Lindi hususan eneo la Mbagala.
Bashungwa amepokea ombi la Mkuu wa Mkoa wa Pwani la kupandisha hadhi barabara ya Vikindu – Vianzi – Sangatini inayounganisha Wilaya ya Mkuranga na Kigamboni ili iweze kuhudumiwa na Wakala ya Barabara (TANROADS).
Vilevile, Bashungwa amemuelekeza Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Dorothy Mtenga kuhakikisha wanashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Pwani katika usanifu wa upanuzi wa barabara za Mkoa huo ili ziende sambamba na mikakati na mipango ya uboreshaji wa Mkoa ikiwemo ujenzi wa Stendi ya Kisasa ya Mabasi inayotarajiwa kujengwa Mkuranga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa fedha za miradi mbalimbali ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 121.1 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS na TARURA.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ali ameeleza kuwa Wilaya hiyo imepokea fedha nyingi za ujenzi wa shule mpya ambapo katika Kata ya Mwandege Shule za Sekondari za Serikali tatu.
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa Jengo la Utawala, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwandege Bw. Ditrick Hokororo ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kumewezesha zoezi la ufundishaji na ujifunzaji katika Shule hiyo kuwa rafiki kwa wanafunzi na walimu ambapo madarasa mawili yaliyokuwa yanatumika kama ofisi za walimu yamerejeshwa kwenye matumizi ya kawaida kwa wanafunzi.