MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari amewataka wadau kutoka sekta mbalimbali kukabialiana na athari zitakazoweza kujitokeza pamoja na kuchukua hatua stahiki wakati wa mvua za msimu zinatotarijwa kuanza mwezi Novembea 2024 hadi Aprili 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka hapa nchini. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa nane wa wadau wa utabiri wa mvua za Msimu uliofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 24/10/2024.
“Mvua za Msimu, Novemba 2023 hadi Aprili 2024 zilitawaliwa na uwepo wa hali ya El Niño. Hali hii ilisababisha uwepo wa matukio ya mvua kubwa katika maeneo mengi nchini. Hivyo napenda kutoa msisitizo kuwa, katika majadiliano ya mvua za Msimu ya mwaka huu, Novemba 2024 hadi Aprili 2025, tujikite katika kujadili athari zinazoweza kujitokeza na kutoa ushauri stahiki”. Alisema Jaji Mshibe.
Jaji Mshibe aliongeza kuwa, Bodi itaendelea kuisimamia vizuri TMA katika utekelezaji wa mipango yake na kuiwezesha kutimiza ipasavyo Dira na mpango mkakati wake ili kuendelea kusaidia maendeleo ya nchi na Dunia kwa ujumla wake. Aidha, aliipongeza TMA kwa kuendelea kutoa utabiri wenye viwango vya juu vya usahihi unaokubalika kitaifa na kinmataifa.
Awali, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Ubora TMA, Dkt. Geofrid Chikojo alisema Mamlaka imeendelea kuboresha taarifa za hali ya hewa kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali, katika kuboresha taarifa hizo kwa wadau, TMA imeendelea kutoa taarifa za utabiri wa maeneo madogo kwa wilaya zote za mikoa iliyopo katika ukanda unaopata mvua za Msimu.
“Utabiri wa Wilaya 63 umeandaliwa kwa maeneo husika, hivyo ni vyema kila wilaya na kila sekta ikatumia taarifa hizo katika kufanya maamuzi na kuweka mipango ili kuboresha huduma zao kwa lengo la kuongeza tija na pia kupunguza madhara ya hali mbaya ya hewa yanapojitokeza”. Alifafanua Dkt. Chikojo.
Naye mwakilishi wa wadau kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Cosmas Makomba alieleza namna taarifa za awali za mvua za msimu 2023/24 zilivyosaidia katika kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuandaa mkakati wa maafa, kutoa mafunzo pamoja na kuandaa mpango wa dharura kwa mikoa iliyotarajiwa kuathirika.
Mkutano huu ni muendelezo wa sehemu ya ushirikishwaji wadau wakati wa maandalizi ya utabiri wa msimu husika ambapo wataalamu kutoka sekta mbalimbali, wanapatiwa fursa za kuona rasimu ya utabiri husika na kutoa michango yao juu ya athari zinazotarajiwa katika sekta husika pamoja na ushauri ili kuwezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari hizo. Aidha, TMA hutumia fursa hiyo kupokea mrejesho wa namna bora ya kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.
Mamlaka inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba 2024 hadi Aprili 2025 kwa maeneo ya Dodoma, Singida, Tabora, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Morogoro Kusini na Kigoma tarehe 29 Oktoba 2024. Kauli mbiu ya msimu huu ni ‘Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa wote na kwa wakati’.