*Ni katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,w waonywa wapika takwimu za uongo.
Na Chalila.Kibuda
OFISI ya Taifa ya Takwimu(NBS) imesema taarifa ya serikali idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, mwaka huu ni sahihi.
Hayo amesema Mtakwimu Mkuu wa NBS Dkt.Albina Chuwa baada ya siku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa kutoa taarifa juu ya matokeo ya zoezi la uandikishaji wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.
Amesema taarifa ya Serikali ilionesha kuwa, wananchi waliojiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo ni 31,282,331 sawa na asilimia 94.83 ya watu wote wenye umri wa kujiandikisha kwa mwaka 2024.
Dkt.Chuwa kumekuwepo na upotoshaji baadhi ya ya mitandao ya kijamii tangu kutolewa kwa taarifa hiyo kwa kudai takwimu zilizotolewa kwamba wananchi walioandikishwa hazina uhalisia takwimu ya watu waliojiandikisha na kwamba idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya watu wanaostahili kujiandikisha kupiga kura inayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Dk. Albina alisema takwimu wanazozizungumzia watu hao ni takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kwamba ulinganishaji wanaoufanya hauendani na hali halisi ya idadi ya watu wenye sifa za kujiandikisha kupiga kura mwaka huu.
Alisema kwa hesabu za kawaida idadi ya watu nchini kwa mwaka 2022 haiwezi kulingana na idadi ya watu kwa mwaka 2024 kwani hivi sasa tayari miaka miwili kamili imeshapita tangu imkufanyika kwa sensa hiyo.
Amesema kutokana na makadirio ya idadi ya watu kwa 2024, idadi ya watu nchini inakadiriwa kuwa Milioni 66.3 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 3.2 kwa mwaka kama ilivyopatikana kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Makadirio haya kwa Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia watu milioni 64.2 na kwa Tanzania Zanzibar yanakadiriwa kufikia watu milioni 2.03, kwa makadirio haya, wananchi tunapaswa kufahamu kuwa idadi ya watu kwa mwaka 2024 haiwezi kuwa sawasawa na ile ya mwaka 2022,” amesema.
Dkt. Chuwa amesema watu waliokuwa na umri wa miaka 16, 17 na 18 katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivi sasa wana umri wa miaka 18, 19 na 20 ambao idadi yao ni 3,785,036 waliokidhi kigezo cha umri wa kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka huu kwa kuwa wana vigezo na sifa za kupiga kura.
Amesema idadi ya watu wenye umri wa kupiga kura ni sawa na watu wote ambao mwaka 2022 walikuwa na umri wa miaka 16 na zaidi ama kwa lugha nyingine ni wote ambao ifikapo Novemba 27, mwaka huu, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 au zaidi.
“Kwa hesabu hiyo inatokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, makadirio ya idadi hiyo ya watu wenye umri wa kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ni watu 32,987,579 ni sahihi na ni rasmi kulingana na Kanunuzi za Msingi za Umoja wa Mataifa Kuhusu Takwimu Rasmi na kama ilivyoripotiwa kwenye taarifa ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI,” alisema.
Dkt.Albina amesema kuhusu kiwango cha uandikishaji kwa mikoa, imejitokeza baadhi yake kuwa na asilimia zaidi ya 100 ya watu walioandikishwa na kufafanua kuwa watu wana tabia ya kuhamahama kutoka eneo moja kwenda eneo na kusababisha uandikishaji wa watu wengi zaidi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa baadhi ya mikoa.
“ Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ilihesabu watu kulingana na mahali walipolala usiku wa kuamkia siku ya Sensa yaani Agosti 23, 2022. Kwa hivyo, hili ni jambo la kawaida na linalowezekana kutokea kama ilivyotokea katika mikoa hiyo ya Pwani (asilimia 112.61); Tanga (asilimia 110.82); Mwanza (asilimia 106.58); Dodoma (asilmia 104.19) na Iringa (asilimia 100.54),” alisema.
Amesema idadi kubwa ya watu mkoa wa Pwani inatokana na watu wengi wa Dar es Salaam kuwa na makazi mkoa wa Pwani hasa katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga. Kwa hiyo ongezeko hilo la watu kwenye maeneo hayo linachangiwa na kuhama kwa watu na si kwa kuandikisha watu waliokosa sifa.
Mikoa yenye asilimia ndogo ya uandikishaji ni ile ambayo chambuzi za kitakwimu zinaonesha ni mikoa yenye uhamaji mkubwa wa watu kwenda katika majiji.
Dk. Albina alitoa takwimu za sensa kwa makundi ya umri na kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watoto walio na umri chini ya miaka 15 nchini ilikuwa 26,399,989 sawa na asilimia 42.8.
Pia idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi wenye umri miaka 15 hadi 64 walikuwa 33,000,128 sawa na asilimia 53.4 na idadi ya wazee walikuwa 2,341,003 sawa na asilimia 3.8.
Amesema wastani wa watoto chini ya umri wa miaka 15 kuwa ni asilimia 60 hadi 70 ni upotoshaji mkubwa kwani hata viwango vya Afrika, asilimia ya watoto ni kati ya asilimia 40 hadi 45 na si vinginevyo.
“Hizi ndizo takwimu rasmi za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura 351 kwa maana hiyo, taarifa iliyotolewa na Serikali ya Idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 ni sahihi kwa sababu kiujumla idadi ya watu wote waliojiandikisha nchini haijavuka ile inayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022,” amesema
Amesema takwimu hizo hazina mashaka yoyote na kuonya kutopotosha umma kwani ni kosa kisheria kupotosha umma kwa kutumia takwimu rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu.
Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara, Spika Mstaafu Anne Makinda aliwataka Watanzania kuacha upotoshaji kwani takwimu zilizopo ni sahihi na zimefuata vigezo vyote.
“Hii ndio taarifa rasmi, takwimu za sensa ndio msingi wa kufanyia kitu kama zisingekuwepo tusingepata asilimia, takwimu za sensa ni mwongozo wa kufanya mambo yote ya maendeleo,” alisema.
Mtakwimu Mkuu wa Ofisi Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt.Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na picha halisi ya Takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kamisaa wa Sensa na Spika wa Bunge Mstaafu Anna Makinda akitoa ufafanunuzi juu ya Takwimu za Sensa zinavyoweza kutumika katika maeneo mbalimbali.
Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Balozi Mohamed Haji Hamza akizungumza kuhusiana namna sensa inavyotoa dira katika masuala mbalimbali zikiwemo chaguzi , jijini Dar es Salaam.