Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Dkt. Nkundwe Mwasaga akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2025, Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa Tuzo za TEHAMA 2025 zinazotarajiwa kufanyika Februari 21, 2025 jijini Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed Mashaka akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2025, Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa Tuzo za TEHAMA 2025 zinazotarajiwa kufanyika Februari 21, 2025 jijini Arusha.
Afisa Miundombinu wa Chama cha Watoa Huduma za Mtandao Tanzania (TISPA) , Joseph Rwegoshora akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2025 kuhusu uzinduzi wa Tuzo za TEHAMA 2025 zinazotarajiwa kufanyika Februari 21, 2025 jijini Arusha.
Mwanzilishi wa Kampuni ya SoftVentures, Daniel Mhina akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2025 kuhusu uzinduzi wa Tuzo za TEHAMA 2025 zinazotarajiwa kufanyika Februari 21, 2025 jijini Arusha.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Tume ya TEHAMA kwa kushirikiana na SoftVentures, Chama cha Watoa Huduma za Mtandao Tanzania (TISPA) imezindua Tuzo za TEHAMA 2025, zinazotarajiwa kufanyika Februari 21, 2025, Jijini Arusha.
Katika tuzo hizo washiriki wametakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia www.tehamaawards.tz hadi Februari 10, 2025 ambapo kutakuwa vipengele 10 zinazotoa fursa kwa wabunifu, wadau wa TEHAMA , Taasisi za Sekta ya umma na binafsi pamoja na Mashirika kushiriki katika kuwania tuzo hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2025 jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa Tuzo za TEHAMA 2025 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kuwa tuzo hizo zinalenga kutambua mchango mkubwa katika sekta ya TEHAMA ya Tanzania, kwa kuwatambua watu binafsi, mashirika, na miradi inayochochea mabadiliko ya kidigitali, kuimarisha ubunifu pamoja na kukuza ushirikishwaji.
Dkt. Mwasaga amesema kuwa hafla ya tuzo za TEHAMA itakuwa jukwaa muhimu kwa viongozi wa sekta, watunga sera, na wabunifu kushirikiana, kuungana pamoja na kuharakisha ukuajiwa uchumi wa kidigitali nchini.
“Mbunifu yeyote anaweza kujisajili au kumsajilia mtu ambaye unamfahamu, wataalamu watachakata na mwisho kumpaa mshindi na kutambuliwa siku ya Tuzo na mwisho wa usajili ni Februari 10, 2025” amesema Dkt. Mwasaga.
Dkt. Mwasaga ametaja vipengele vinavyoshindaniwa katika tuzo za TEHAMA 2025 kuwa ni Ubunifu katika Bidhaa au Huduma za TEHAMA, Matumizi Bora ya TEHAMA, TEHAMA kwa Maendeleo ya Jamii, Kijana Aliyefanikiwa Katika TEHAMA.
Vipengele vingine ni Wanawake Katika TEHAMA, Usalama wa TEHAMA, Mradi wa TEHAMA wa Sekta ya Umma, TEHAMA Endelevu, Tuzo za TISPA kwa Mtoa Huduma Bora ya Uunganishaji wa Mtandao pamoja na Tuzo Maalum ya Maisha kwa Mchango wa TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari.
Amesema kuwa jumla ya tuzo 22 zinatarajiwa kutolewa siku ya kilele, huku akiwakaribisha wadau mbalimbali na wawekezaji kujumuika pamoja katika Tuzo hizo.
Afisa Miundombinu TISPA, Joseph Rwegoshora amesema kuwa TISPA ni chombo cha sekta kinacho wakilisha watoa huduma za mtandao na wadau wa TEHAMA kwa kutetea ushirikishwaji wa kidigitali, maendeleo ya sera, na upanuzi wa miundombinu ya TEHAMA ili kusaidia ukuaji wa uchumi.
Mwanzilishi wa Kampuni ya SoftVentures, Daniel Mhina ameeleza umuhimu wa tuzo hizo kwani vitakuwa za kipikee na endelevu pamoja na kuhakikisha miaka ijayo zitaendelea kuwa nzuri zaidi.