Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo katika kikao cha Baraza la wafanyakazi kilichofanyika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani Januari 24, 2025.
Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Zella Rwemanyira akizungumza na watumishi wenzake katika kikao hicho.
…………………
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, amesisitiza umuhimu wa mchango wa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kufanikisha maboresho makubwa yanayopangwa katika ofisi hiyo. Maboresho haya ni pamoja na kuboresha miundombinu, kuimarisha vifaa vya kisasa vya kazi, na kukarabati ofisi zilizopo katika mikoa tisa nchini.
Akizungumza Januari 24, 2025, wakati wa kufunga kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kilichofanyika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani, Mhe. Johari alitambua jitihada za watumishi katika kuhakikisha ufanisi wa kazi unapatikana.
Alisema, “Michango ya kila mtumishi ni muhimu sana katika kuhakikisha tunafanikisha maboresho haya. Tunategemea utendaji kazi wenu wenye bidii ili kuyafanya mabadiliko haya kuwa ya manufaa makubwa kwa taifa.”
Kwa upande wa maendeleo ya miundombinu, Johari alibainisha kuwa hatua za kukamilisha Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma zinaendelea kwa kasi. Jengo hilo litakuwa na ukumbi wa mikutano wa kisasa na miundombinu inayowiana na mahitaji ya kiteknolojia ya sasa.
Aidha, alieleza kuwa vifaa kama kompyuta mpakato na kishikwambi vitawasaidia watumishi kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kila siku. Hata hivyo, alisisitiza kwamba ubora wa mazingira ya kazi pekee hautoshi, bali watumishi wanapaswa kuonyesha juhudi binafsi katika kutimiza majukumu yao kwa weledi na bidii.
Johari pia aliwapongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa mchango wao mkubwa katika kusimamia sheria na kuchochea mabadiliko chanya nchini, akisema, “Watumishi wetu ni nguzo muhimu katika kuhakikisha tunaendelea kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya sheria nchini.”
Kauli hii inaonyesha jinsi viongozi wanavyotambua nafasi ya watumishi katika kuboresha utoaji wa huduma bora kwa taifa, huku wakichochea bidii zaidi katika utendaji kazi wa kila siku.
Nae Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Zella Rwemanyira ametoa rai kwa watumishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuendana na dhana ya Weledi na Ubora.
“Natoa rai kwa Watumishi wenzangu wa Ofisi ya Mwanasheria kuendelea kuchapa kazi kwa bidi ili tuendane na dhana ya Weledi na Ubora.” Amesema Bi. Zella.