Farida Mangube, Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Mussa Ali Mussa, amewahimiza watafiti kuchapisha matokeo ya tafiti zao kwa Kiswahili ili kuhakikisha jamii inayolengwa inanufaika moja kwa moja na utafiti huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa utafiti wa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Mussa alisema tafiti nyingi zimekuwa zikiandikwa kwa lugha za kigeni, hali inayowakwamisha wafugaji na wananchi kwa ujumla kunufaika na matokeo hayo.
“Serikali inatumia rasilimali nyingi kufadhili tafiti hizi, lakini matokeo yake hayafikii jamii kwa lugha inayoeleweka. Hili linaifanya jitihada ya tafiti hizi kupoteza umuhimu wake,” alisema Bw. Mussa.
Alisisitiza umuhimu wa watafiti kushirikiana na watunga sera ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatengeneza miongozo na sheria zitakazosaidia kuimarisha maisha ya jamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka SUA, Prof. Esron Karimuribo, alisema mradi huo unalenga kudhibiti na kuzuia magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, ambayo yanaathiri si tu afya ya watu na mifugo, bali pia uchumi wa jamii. Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri tisa za Mkoa wa Morogoro.
“Magonjwa haya huathiri mifugo na binadamu, na hatimaye kushusha pato la kaya na uchumi wa jamii kwa ujumla,” alisema Prof. Karimuribo.
Baadhi ya wafugaji wa Mkoa wa Morogoro walieleza changamoto ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) unaotokana na ng’ombe, ambao umeenea kwa kasi, hasa kutokana na uhamaji wa mifugo.
Dkt. Kohei Makita, Mratibu wa mradi wa JICA, alisema tafiti kuhusu TB katika mifugo zilianza kufanyika Tanzania tangu mwaka 2008, lakini changamoto kubwa bado ni ukosefu wa uelewa kwa wafugaji.
“Wafugaji wengi hawana uelewa kwamba TB inaweza kuambukizwa kutoka kwa ng’ombe kwenda kwa binadamu, hali inayochangia kusambaa kwa ugonjwa huu,” alisema Dkt. Kohei.
Bw. Kochocho Mgema, mfugaji kutoka Morogoro, alikiri kuwa ugonjwa wa TB ni changamoto kubwa kwao, lakini wengi wa wafugaji hawaelewi chanzo chake.
Kupitia mradi huu, wataalamu wanapendekeza mikakati madhubuti kama kutoa elimu kwa wafugaji, kudhibiti uhamaji wa mifugo, na kuimarisha huduma za afya ya mifugo ili kudhibiti magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Serikali, kwa kushirikiana na SUA na JICA, inatarajia kuwa mradi huu utaimarisha si tu afya ya mifugo na binadamu, bali pia kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Morogoro kupitia sekta ya mifugo.