Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imejipanga kufanya maboresho makubwa ya uendeshaji wa Shule 71 zinazomilikiwa na Jumuiya hiyo kwa kuweka mkakati ya kuhakikisha shule hizo zinakuwa na viwango bora kwa kuingia ubia na wawekezaji ambao wataleta tija kwa kutoa huduma bora ya elimu.
Akizungumza leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam katika Kikao na Wawekezaji katika Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Bw. Fadhili Maganya, amesema kuwa baadhi ya Shule za Jumuiya zimekuwa zikijiendesha kwa mafanikio, huku nyengine zikisuasua.
Bw. Maganya amesema kuwa ili kupata mafaniko wameona ni vyema kufanya kikoa na wawekezaji katika seka ya elimu ili kubainisha fursa zilizopo na kufanya kazi pamoja kwa njia ya ubia katika kuendesha shule hizo kwa makubaliano.
“Tumekutana na Bodi za Shule na Vyuo mbalimbali wakiwemo wanawake wawekezaji katika sekta ya elimu, wamiliki wa shule binafsi, Vyama vya Wakuu wa shule ambapo tumezungumza nao na kufungua milango ya kushirikiana nao kama tutakubaliana nao ” amesema Bw. Maganya.
Amefafanua kuwa kanuni za jumuiya ambazo zinatokana na katiba ya chama cha mapinduzi inawapa jukumu la kushughulika na elimu, hivyo kikao hicho na wadau wa sekta ya elimu ni sehemu ya kutafuta namna bora ya kuendesha shule hizo, huku akiwakumbusha wawekezaji ambao wamepewa jukumu la kuendesha shule kuongeza ufanisi.
“Tofauti na uendeshaji wa shule, jumuiya ina mpango wa muda mfupi wa kufanya uwekezaji wa kuanzisha Hospitali ya rufaa pamoja na kujenga hospitali ya Mama na mtoto Pemba na hospitali nyingine Mkoani Iringa” amesema Bw. Maganya.