NA FAUZIA MUSSA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeda Rashid Abdalla, amesema kuwa uwepo wa majukwaa ya kumuwezesha mwanamke kiuchumi utawasaidia wanawake kujitegemea na kuepuka kuwa tegemezi kwa familia.
Abeda alitoa kauli hiyo wakati akitoa elimu kwa vikosi kazi vinavyotarajiwa kuanzisha majukwaa hayo katika kila shehia, huko Tunguu, kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja. Alisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa zoezi hilo ili kuhakikisha wanawake wote wanapata fursa ya kunufaika.
Alisema kuwa lengo la majukwaa hayo ni kuleta mageuzi chanya ya kiuchumi kwa wanawake wa Zanzibar, kwa kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akihimiza juhudi za kuanzisha mifumo hiyo ili kuwawezesha wanawake kupata fursa za maendeleo.
“Ni wakati sasa wa kufanya kazi kwa pamoja katika kuanzisha majukwaa haya kwa haraka zaidi kama ilivyoelekezwa na mwanamke mwenzetu, mama yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, *Dk. Samia Suluhu Hassan,” alisisitiza Abeda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abasi Ali, aliahidi kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mpango huo, akieleza kuwa wanawake wa Zanzibar hawapaswi kukosa fursa hizi.
“Wenzetu Tanzania Bara tayari wameanza kunufaika na majukwaa kama haya. Hatupo tayari kuipoteza fursa hii. Tutahakikisha majukwaa yanaundwa na yanatekelezwa ipasavyo,” alisema Siti.
Alifafanua kuwa majukwaa hayo yanalenga kuweka mazingira bora kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi na kupata fursa sawa na wanaume katika jamii.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Unguja, Radhia Rashidi Harub, alieleza kuwa majukwaa hayo ni nyenzo muhimu kwa wanawake kupata rasilimali, elimu, na mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi ili kujikwamua kutoka katika utegemezi.
“Tunahitaji kulipa suala hili kipaumbele ili kila mwanamke aweze kuanzisha au kuimarisha shughuli zake za kiuchumi na kupata maendeleo,” alisema Radhia.
Majukwaa haya yameanzishwa kwa malengo ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uchumi, kuwawezesha kupata fursa sawa, na kuleta usawa wa kijinsia katika masuala ya kijamii na kiuchumi.