WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Mkesha Maalum wa kuombea Taifa na kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 ulioandaliwa na Kanisa la Heavenly Image Manifest (HIM) chini ya Nabii Edmund Mystic.
Mkesha huo unaotarajia kufanyika Februari 28, mwaka huu, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, utakaohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari juu ya mkesha huo wa maombi, Nabii Edmund amesema kwa Tanzania mwaka 2025 ni moja ya mwaka muhimu kwa Taifa kwasababu ya tukio kubwa la uchaguzi mkuu.
Amesema kanisa lina nafasi ya kulibeba Taifa kwa namna moja na nyingine kwa kufanya maombi hivyo kupitia maombi hayo yatahusisha pia kumwombea Rais Samia kwasababu yeye ni mtawala na amebeba hatima kubwa ya Watanzania.
Amesema hawawezi kuombea serikali wanayoitazamia kwenye uchaguzi ujao pasipo kuanza na serikali iliyopo madarakani hivyo ni lazima kumwombea Rais Samia ambaye Mungu alimuweka kwenye kiti cha Urais.
“Kila Mtanzania ana nafasi ya kusimama na kuiombea Taifa la Tanzania kwa imani yake na kile Mungu atakachompa kuombea kwa sababu biblia imesema.
“Habari ya kuombea Tanzania ni suala nyeti ambalo Mungu anaenda kuikumbuka nchi na kuirehemu, kama kuna makosa tumefanya alafu tukasimama kuomba rehema kwa Tanzania Mungu ana uwezo wa kufanya kitu, maombi ni kitendo cha unyenyekevu na tuna muhitaji Mungu aingilie kati katika haya,”amesema Nabii Edmund.
Amesema Mungu aliwaagiza Februari 28 ni siku ya kutengeneza matokeo ya nchi ya Tanzania Bora, hivyo kuna umuhimu wa Watanzania kusimama na kutengeneza kesho ya nchi yetu kwa maombi.
“Tumeona mwaka jana kwa habari ya Kenya kulivyotokewa na machafuko ambapo watumishi wa Mungu walihubiri hivyo hivyo, tunaposikia unabii umetolewa na Mtumishi wa Mungu tusiutweze unabii huo,”amesisitiza.
Kuhusu uchaguzi, Nabii Edmund, alitoa rai kwa Watanzania wanaoenda kuingia katika uchaguzi kuepuka na chochote ambacho kinaweza kuhatarisha hali ya usalama kwa Watanzania.
Amesema wanapaswa kutotegemea waganga wa kienyeji katika uchaguzi mkuu unaelekea kufanyika Oktoba mwaka huu kwasababu kwenye biblia imeandikwa amelaaniwa yule amtegemeae mwanadamu ni vema kumtegemea Mungu.
“Msimtegemee mganga wa kienyeji kumekuwa na kitu ambacho watu hawakifahamu mganga wa kienyeji anamsaidia mwanasiasa kushinda kwa sababu ya kitu kinaitwa kusimamisha madhabahu ya rohoni,”amesema.
Aidha, amesema wanasiasa watakaogombea wanapaswa kuzingatia uchaguzi unaosimamia haki na sheria ambazo zimeweka nchini.
“Ifike mahali kupata uchaguzi ambao umenyooka na kuwa na uchaguzi huru na wa haki ambaye ni yule Mungu amemkusudia ndiye asimamia na kukaa katika nafasi yake,”amesisitiza Nabii Edmund.