………………………
Sixmund Begashe -Ngorongoro
Jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kutatua changamoto ya Mimea Vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria nchini zitakwenda kuzaa matunda pindi lengo la kubadili mimea hiyo na kuwa bidhaa kwaajili ya Matumizi ya binadamu na za kumaliza mimea hiyo kwenye maeneo hayo yenye malisho ya Wanyamapori.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Cuba Mhe. Humphrey Polepole katika Hifadhi ya eneo la Ngorongoro alipoongozana na timu ya Watafiti wa mimea vamizi kutoka Cuba na wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mhe. Polepole amebainisha kuwa wingi wa mimea vamizi iliyoonekana katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inafanana na ya nchini Cuba, hii ni kutokana na mlingano wa hali ya hewa kwa asilimia kubwa hivyo wa Cuba waliitumia changamoto hiyo kama fursa kwa kutumia mimea hiyo kutengenezea bidhaa mbalimbali kwa Matumizi ya binadamu.
“Wenzetu wa Cuba, walikuwa na changamoto tuliyonayo hapa, wakaibadlisha kuwa fursa kwa kutengeneza dawa za kudhibiti mimea vamizi kwenye Hifadhi na bidhaa zinazotumika na binadamu ndio maana tumeona tushirikiane na wataalam hawa ili na sisi hapa nchini tutumie utaalam huo kuifanya changamoto hii kama fursa” Amesema Mhe. Polepole
Aidha ameongeza kuwa, mashirikiano hayo ya Cuba na Tanzania kupitia watafiti hao yatakwenda kuiweka Tanzania kuwa nchi inayoongoza katika kutafuta suluhu ya changamoto hiyo na kutoa nafasi kwa nchi zingine kuja kujifunza nchini.
Mhe. Polepole amefafanua kuwa, uwepo wa timu hiyo watafiti kutoka nchini Cuba ni sehemu ya utekelezaji wa magizo ya Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha mashirikiano ya kimataifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya Uhifadhi wa Maliasili nchini kazi iyofanywa vyema na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wakiwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mhe. Balozi Polepole na watafiti hao, wametembelea maeneo ya Kayapus, Kakesio na Tambarare za ndutu na kushuhudia mimea vamizi kwa majina ya kitaalam ijulikanayo kama Parthenium hysterophus (Gugu karoti, Gutenibergia cordifolia (Gutenbergia), ilivyoathiri ikolojia ya ya Hifadhi hiyo.