Na WAF, MWANZA
Msajili wa Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi amewataka wamiliki wa vituo vinavyotoa huduma za optometria vikiwemo kliniki, maabara , wasambazaji wa bidhaa za miwani tiba, fremu za miwani na lenzi tiba kutoa huduma bora kwa jamii kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuilinda jamii.
Bw. Millanzi ametoa rai hiyo Februari 19, 2025 wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi kwa kuwakumbusha wamiliki wote wajibu wanaotakiwa kuutekeleza kabla ya kuanza kutoa huduma hizo.
“Ili kulinda afya ya macho ya jamii yetu ni marufuku kituo chochote kutoa huduma za optometria bila ya kuwa na mtaalam wa Optometria aliyesajiliwa na Baraza la Optometria na aliye na leseni hai, kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na atakayebainika hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, ” amesema Bw. Millanzi.
Bw. Millanzi ambaye ameongoza jopo la wataalam kutoka Wizara ya Afya amefanya zoezi hilo katika vituo mbalimbali vilivyopo mkoani Mwanza ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, St. Clara, Hospitali ya Kamanga na Kalisa Optometry Centre .
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Millanzi amewakumbusha wamiliki wa vituo vinavyotoa huduma ya optometria kuhakikisha hawawatumii watu wasio na taaluma hiyo yaani (Vishoka) kutoa huduma hizo.
“Baraza lipo kwa ajili ya kuwasimamia wataalam wa optometria ikiwemo kuwasajili, mara baada ya kukidhi vigezo vikiwemo kuhitimu mafunzo ya optometria kwa ngazi ya Stashahada au zaidi katika vyuo vilivyo na sifa na kufaulu, hivyo tukikuta watu wanatekeleza majukumu hayo bila ya kuwa na utaalam watachukuliwa hatua ikiwemo kufunga kituo husika,” amesisitiza Bw. Millanzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamiliki wa vituo wamekiri kupokea ushauri na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zilizopo.
Bw. James Apollo ambaye ni Katibu wa Afya katika Hospitali ya St. Clara iliyopo Nyahingi amekiri uwepo wa Mapungufu na kuahidi kuchukua hatua za dharura ili kutatua tatizo linalowakabili ikiwepo kuajiri mtaalam aliyefuzu mafunzo ya Optometria.