Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Othuman akifunga mkutano wa viongozi wa mashirika na viwanda vya kijeshi vya EAC uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Girrafe jijini Dar es Salaam Februari 26, 2025.
………………
Dar es Salaam – Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imehimizwa kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha viwanda vya kijeshi ili kuongeza uwezo wa kujitegemea katika sekta ya ulinzi na kupunguza utegemezi wa masoko ya kimataifa.
Akifunga mkutano wa viongozi wa mashirika na viwanda vya kijeshi vya EAC jijini Dar es Salaam, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Othuman, alisema ushirikiano wa kikanda utasaidia kuongeza ushindani dhidi ya kampuni kubwa za kimataifa zinazozalisha zana za kijeshi.
“Ili kuimarisha sekta ya viwanda vya ulinzi, ni muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana katika teknolojia, rasilimali na utafiti. Hii itasaidia kanda kujitegemea na kupunguza changamoto zinazotokana na utegemezi wa masoko ya nje,” alisema Luteni Jenerali Othuman.
Mkutano huo, ulioshirikisha wajumbe kutoka nchi nane za Afrika Mashariki na majeshi 80, ulijadili njia za kuimarisha viwanda vya kijeshi kwa ushirikiano wa kikanda.
Viongozi walibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa zinazokabili viwanda hivyo ni ukosefu wa teknolojia za kisasa na rasilimali za kutosha. Walisisitiza kuwa uwekezaji katika sayansi, teknolojia na utafiti ni hatua muhimu ili kuhakikisha viwanda vya ulinzi vinakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya kanda.
“Mara nyingi ununuzi wa vifaa vya kijeshi kutoka nje huambatana na masharti magumu yanayodhoofisha uwezo wetu wa kuvitumia kikamilifu. Ushirikiano wa kikanda utasaidia kupunguza utegemezi huu na kuongeza ubunifu wetu katika sekta ya ulinzi,” aliongeza Luteni Jenerali Othuman.
Mkutano huo uliambatana na maonyesho ya viwanda vya ulinzi, ambapo Tanzania iliwasilisha mafanikio yake katika kukuza viwanda vya kijeshi. Washiriki walipata fursa ya kuona maendeleo ya kiteknolojia yanayofanywa na sekta ya ulinzi ya Tanzania, hatua inayoimarisha uwezo wa nchi kujilinda na kukuza uchumi wa kanda.
Kwa mujibu wa viongozi wa mkutano huo, viwanda vya kijeshi vina mchango mkubwa si tu katika usalama, bali pia katika maendeleo ya kiuchumi kwa kuzalisha ajira na kuongeza uzalishaji wa ndani.
Katika hotuba yake ya kufunga mkutano, Luteni Jenerali Othuman aliwasihi viongozi wa viwanda vya kijeshi kutoangalia mafanikio ya haraka, bali kujikita katika kujenga misingi thabiti kwa maendeleo endelevu.
“Maendeleo ya viwanda vya kijeshi ni jambo la muda mrefu. Tunapaswa kuwa wavumilivu, kushirikiana na kuhakikisha kuwa tunajenga msingi imara wa viwanda vyenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya ndani na ya kikanda,” alisema.