Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Fatma Mabrouk Hassan amewataka Vijina kuenda na wakati kwa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ili waweze kujikomboa kimaisha.
Ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya pili ya Kituo cha Maendeleo ya Vijana, kilichopo Bweleo Wilaya ya Magharibi ‘B”.
Amesema Serikali inakusudia kujenga vituo vya kisasa katika kila Mkoa ili kusaidia Vijana kupata mafunzo mbalimbali, yatakayowasaidia kupata ajira na kuendesha maisha yao ya kila siku.
Aidha amesema pia Serikali imezindua Sera mpya ya Maendeleo ya Vijana ili kusaidia Wadau katika kufikia maendeleo ya Vijana kwa haraka.
Aidha amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza tatizo la ajira katika jamii
Hata hivyo amewataka Vijana wasibweteke watumie mbinu mbadala na za kiasasa ikiwemo mitandao ya Kijamii ili waweze kukuza Ujuzi na kufikia malengo yaliokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar Shaibu Ibrahim Muhamed amesema Mafunzo hayo yanasaidia Vijana kuwa Wazalendo katika kuleta maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mbali na hayo amesema lengo la vituo hivyo ni kuweka miundombinu rafiki itakayowawezesha Vijana kusoma fani mbalimbali ikiwemo za Ujasiriamali.
Akisoma Risala katika Mahafali hayo, Mwanafunzi wa fani ya Ushoni Asha Ame Mwadini amesema wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kukosa mitaji ya kuanzisha Miradi hivyo wameiomba Serikali, Wadau na Watu wenye uwezo kuwasaidia ili waweze kuanzisha miradi Yya maendeleo wakati watakapomaliza mafunzo.
Kituo Cha Maendeleo ya Vijana Bweleo Wilaya ya Magharibi B, kimeanzishwa mwaka 2023, kina jumla ya Vijana 1,021 Wanawake 658 na Wanaume 363 na kinatoa Mafunzo ya fani mbalimbali ikiwemo Stadi za Maisha, Uongozi, Aluminium na Ushoni.
Imetolewa na Kitengo Cha Habari,
WHVUM.