Na Prisca Libaga Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameonya wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha kujiepusha na upandishaji wa Gharama za vyakula vinavyotumika zaidi wakati huu wa msimu wa mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhan, akitangaza kuja na Operesheni maalum ya kutembelea maduka ili kubaini wafanyabiashara wanaotumia mfungo wa Ramadhan kujitafutia faida ya ziada.
“Niwasihi, mwezi huu ( Mwezi mtukufu wa Ramadhan) sio mwezi wa kutengeneza faida, mwezi huu ni wa kutafuta baraka, faida unayoitafuta inaweza kuna kukugharimu sana, ukajikuta umepata magonjwa yakala mpaka na mtaji wako. Wenzako wanapofunga kwaajili ya kumuomba Mwenyenzi Mungu, jitahidi na wewe uwe sehemu ya baraka ya kuhakikisha kuwa huwapi vikwazo.” Amesema Mhe. Makonda.
Mhe. Makonda pia kando ya kuarifu kuwa Mkoa unaandaa futari kwaajili ya wananchi wa Mkoa wa Arusha, amewatakia Kheri pia Waislamu wa Mkoa wa Arusha kwenye mfungo waliouanza mwishoni mwa Juma lililopita sambamba na kwa Wakristo ambao wanatarajiwa kuanza mfungo wa Kwaresma hivi karibuni, akiomba kuwa funga zao zikafanyike kuwa baraka na kichocheo cha amani na Upendo katika Mkoa wa Arusha.








