Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs
Mwambegele akizungumza leo Machi 05,2025 wakati akifungua mkutano wa
Tume na Wadau wa uchaguzi mkoa wa Dar es Salaam kuhusu Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs
Mwambegele akizungumza leo Machi 05,2025 wakati akifungua mkutano wa
Tume na Wadau wa uchaguzi mkoa wa Dar es Salaam kuhusu Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Ndg. Kailima, R. K
akiwasilisha mada kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura leo Machi 05,2025 wakati mkutano wa Tume na Wadau wa uchaguzi mkoa
wa Dar es Salaam.
Sehemu ya wadau walioshiriki mkutano huo leo
Sehemu ya wadau walioshiriki mkutano huo leo
Uboreshaji
wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Dar es Salaam utafanyika kwa
siku saba kuanzia tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025 ambapo wapiga kura
wapya 643,420 wanatarajiwa kuandikishwa.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji
wa Rufani Jacobs Mwambegele na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo,
Kailima Ramadhan kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika jijini
Dar es Salaam leo tarehe 05 Machi, 2025.
“Leo tupo hapa Dar es
Salaam ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa huu,
ambapo zoezi litafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 17 Machi,
2025 na kukamilika tarehe 23 Machi, 2025 na vituo vitakuwa vinafunguliwa
kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema Jaji
Mwambegele.
Amesema mkoa wa Dar es Salaam ndio wa mwisho kwenye
awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Dafatri ambayo ilizinduliwa mwezi
Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeshafanyika
kwenye mikoa 28 na kwamba mikoa ya Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga
inatarajiwa kukamilisha zoezi hilo tarehe 07 Machi, 2025.
“Hadi
leo tarehe 05 Machi, 2025 Tume imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari
katika Mikoa 28. Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi
ya mzunguko wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari.
Mzunguko huu unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Aidha,
zoezi la uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa wa Morogoro na sehemu ya mkoa
wa Tanga kwenye Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na
Mkinga unaendelea tangu tarehe 01 Machi, 2025 na utakamilika tarehe 07
Machi, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
Akiwasilisha
mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu. Kailima
Ramadhan amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam Tume inatarajia kuandikisha
wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya
wapiga kura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Tume
inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na
wapiga kura 4,071,337. Aidha, idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa
inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa
wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa
sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema Kailima.
Ameongeza
kuwa mkoa wa Dar es Salaam una vituo 1,757 vitakavyotumika kwenye
uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96 katika
vituo 1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Kailima
amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari linahusu kuandikisha wapiga kura
wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na
watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,
kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika
na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao
yakiwemo majina na taarifa nyingine.
“Uboreshaji
wa Daftari pia utahusu kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye
Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au
jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za
kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuukana uraia wa Tanzania na kifo,” amesema Kailima.