Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma(Mbifacu)Faraja Komba na Mwenyekiti wa Chama hicho Michael Kanduyu kulia,wakiangalia uzalishaji wa kahawa kwenye shamba la mkulima katika Kijiji cha Malindindo kata ya Mhekela Halmashauri ya Wilaya Mbinga.(Picha na Muhidin Amri).
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Michael Kanduyu kulia,akimuonyesha Kaimu Meneja wa Chama hicho Farja Komba kushoto,wakikagua miti ya kahawa inayoendelea kuzaaa wakati wa ziara ya kutembelea Wakulima wa kijiji cha Malindindo Halmashauri ya Wilaya Mbinga jana,ziara hiyo ililenga kusikiliza changamoto zinazowakabili Wakulima wa zao hilo.
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
WAKULIMA wa zao la kahawa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kutekeleza mpango wa kutoa pembejeo za ruzuku katika msimu wa kilimo 2023/2024/2024/2025 ambao umehamasisha wakulima wengi Wilayani humo kufufua na kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbinga(Mbifacu) Michael Kanduyu amesema,kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa kumetokana na wakulima kuwa na uhakika wa kupata mbolea inayouzwa kwa bei ndogo.
“katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,uzalishaji wa kahawa mashambani umeongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na ruzuku iliyowekwa kwenye mbolea na Serikali ya awamu ya sita”alisema Kanduyu.
Amesema,kupitia mfumo wa ruzuku Wakulima wananunua mbolea aina ya UREA kwa Sh.68,000,CAN Sh.62,000 na SA inauzwa kwa Sh.48 tofauti na awali ambapo bei ilikuwa Sh.150,000 hadi 180,000.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kutoa ruzuku kwenye dawa za kupulizia kahawa kama ilivyo kwa zao la korosho na Pamba ili kuwapunguzia wakulima gharama kubwa za uzalishaji wa zao hilo maarufu hapa nchini.
Mkulima mwingine na mkazi wa kijiji cha Malindindo kata ya Kambarage Lucas Mahay amesema,kupatikana kwa mbolea za ruzuku ni dhahiri Serikali inawathamini sana wakulima kwani baadhi yao walishaanza kukata juu ya upatikanaji wa bidhaa hiyo.
“kabla ya Serikali kuanza mpango wa kutoa mbolea za ruzuku wakulima wengi tulipunguza ukubwa wa mashamba kwa kulima eneo dogo ili kukidhi mahitaji kutokana na bei kuwa juu huku mazao yakiuzwa kwa bei ya chini” alisema Mahay.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa Wakulima wa kahawa na kuwapongeza viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika (Mbifacu)kuanzisha mpango wa kuwakopesha wakulima mbolea ambao umewavutia na kushawishi Wakulima wengi kujiunga na Ushirika.
Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbinga(Mbifacu)Faraja Komba amesema,katika kipindi cha miaka minne chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka wastani wa tani 15,000 msimu 2021/2022 hadi tani 25,000 msimu 2024/2025.
Komba amesema,ongezeko hilo ni mafanikio makubwa kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla kupitia Halmashauri za Wilaya ambazo zimepata zaidi ya Sh.bilioni 5 kutokana na ushuru na tozo mbalimbali kutoka kwenye zao la kahawa.
“kwa hiyo unaona vya msingi vya Ushirika(Amcos)vinavyochangia maendeleo kwa Serikali na mtu mmoja mmoja,vyama hivi vimewekeza miradi mbalimbali kama mashamba,kununua vyombo vya usafiri na kujenga maghala kama miradi inayosaidia kuleta mapato”alisema Komba.
Alitaja mafanikio mengine,ni matumizi sahihi ya pembejeo zinazopatikana kwa bei ya ruzuku,na ameishukuru Serikali kutoa pembejeo kwa bei ya punguzo ambazo Wakulima wanapata kwa urahisi na kuzitumia kwenye mashamba yao.
“miaka ya nyuma bei ya mbolea aina ya UREA tulinunua kwa Sh.110,000 hadi 150,000 mfuko mmoja wa kilo 25, lakini kupitia bei za ruzuku sasa inauzwa Sh.62,000 ambayo kila mkulima ananunua”alisema.
Katika hatua nyingine Komba alisema,wamepanua mtandao wa soko la kahawa na kupitia Ushirika kuna masoko matatu soko la minada,soko la moja kwa moja na soko la mkataba ambapo makampuni na wafanyabiashara wananunua kahawa kupitia Vyama vya Ushirika hivyo kuvisaidia Vyama kukua na kutengeneza mtandao wa biashara.
Alisema,kwa muda wa miaka mitatu wametoa Sh.milioni 999 zilizo kwenda kwenye Halmashauri ili kuboresha huduma za kijamii katika Wilaya ya Mbinga ambayo sehemu kubwa ya uchumi wake inategemea zao la kahawa.
Alisema, katika msimu wa kilimo 2024/2025 wakulima wamelipwa zaidi ya Sh.bilioni 208 baada ya kuuza tani 23,000 za kahawa na bei wastani ni Sh.8,700 lakini baadhi ya maeneo kahawa imeuzwa kati ya Sh.9,000 na 10,000 kwa kilo moja na fedha hizo zimesaidia wakulima kuongeza uchumi wao.
Kuhusu mikopo ya pembejeo Komba alisema,wametoa zaidi ya tani 718 zenye thamani ya Sh.bilioni 1.2 kwenda kwa wakulima na mikopo hiyo italipwa kupitia komo za madeni za pembejeo zilizopo kwenye vyama vya msingi vya ushirika(Amcos).
Alisema,mpaka sasa komo za madeni zilizotolewa kwenye vyama vya msingi ni zaidi ya Sh.bilioni 8 ambazo zinakwenda kufanikisha upatikanaji wa pembejeo na kuongeza uzalishaji.
Afisa masoko wa Mbifacu Osmund Mbunda alisema, Mbifacu inasimamia masoko matatu ambayo ni soko la awali ambalo mkulima anauza kahawa ambayo haijachakatwa na soko la moja kwa moja ambapo mkulima anauza kahawa safi.
Alitaja soko la tatu ni soko la mnada,hata hivyo mkulima ananufaika sana kupitia soko la moja kwa moja kwa sababu soko hilo ni la mkataba kati ya mnunuzi na mkulima hata kama bei ya kahawa inaweza kushuka.