Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi na Majengo wa Wizara, Balozi Said Shaibu Mussa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kujenga na kukarabati majengo ya Balozi zake ili kupunguza gharama za kukodi na kupanga majengo nje ya nchi.
Balozi Mussa ameyasema hayo jijini Harare tarehe 10 Machi, 2025 alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe na kukagua majengo Nane yanayomilikiwa na Ubalozi huo ikiwemo Jengo la Ofisi za Ubalozi na nyumba za Watumishi.
Balozi Mussa ambaye alipokelewa ubalozini hapo na Balozi wa Tanzania Zimbabwe, Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Mhe. Simon Sirro amesema azma ya Serikali ni kuendelea kujenga majengo ya Balozi na vitega uchumi katika nchi mbalimbali ambazo tayari Tanzania inayo maeneo ili kuondokana na gharama kubwa za kukodi.
Amesema tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mifuko ya Jamii kama NSSF na PSSSF inatelekeza miradi mikubwa ya ujenzi wa majengo ya Balozi na vitega uchumi kama wa Nairobi, Kenya na Ukumbi wa kisasa wa mikutano wa kimataifa wa Kilimanjaro utakaojengwa jijini Arusha.
Akiwa Ubalozini hapo, Balozi Mussa amesema anaona fahari na kufarijika kuona Ubalozi unamiliki majengo nane ambayo miongoni mwake jengo moja linatumika kama kitega uchumi.
“Nafarijika kuona majengo haya yote ni ya kwetu, hakuna ambalo tumekodi, hii ni faraja kubwa kwani inatusaidia kama Wizara kupunguza gharama za kutumia fedha nyingi katika kukodi majengo. Tunataka zaidi tupate mapato kutokana na vitega uchumi lakini vilevile kutokana na uwepo wa majengo yetu” alisema Balozi Mussa.
Balozi Mussa pia alitumia nafasi hiyo, kutoa rai kwa watumishi wa Ubalozi huo kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana kwa hali na mali ili kuwezesha malengo ya Serikali kwenye Ubalozi huo kutimia.
“Balozi Sirro anaondoka nyie mtakuwepo, nyinyi ndiyo mtamsaidia Balozi ajaye kutekeleza majukumu yake kikamilifu, Afande Kaganda ni mama hodari wa kazi kwa hiyo mumpatie ushirikiano na mumsaidie” alisisitiza Balozi Mussa.
Pia alipongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Ubalozi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na kuwataka kuendelea kuishauri Serikali kuhusu namna ya kunufaika na fursa na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo baina ya Tanzanja na Zimbabwe.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Sirro ambaye anamaliza muda wake wa utumishi kituoni hapo, amemshukuru Balozi Mussa kwa kutenga muda wake na kuutembelea Ubalozi huo ambapo kwa niaba ya Watumishi, ameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa.
Kadhalika, alieleza kuwa hali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Zimbabwe ni nzuri ambapo nchi hizi zinaendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji na masuala yanayohusu Kanda ya Kusini mwa Afrika.
Balozi Mussa yupo nchini Zimbabwe kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika nchini hapa kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi 2025. Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ambapo Balozi Mussa aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye vikao hivyo.