Na. Faraja Mbise, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejipanga vema kutoa huduma kwa wananchi wote kwa kuzingatia mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini wenye mapendekezo ya kuligawa jimbo hilo kuwa Jimbo la Mtumba lenye jumla ya kata 20 na Jimbo la Dodoma Mjini lenye kata 21.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, mara baada ya majadiliano kutoka kwa Madiwani kuhusu taarifa iliyowasilishwa na Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Albert Kasoga ya kuwasilisha mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani lililofanyika tarehe 12 Machi, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Dkt. Sagamiko alisema “mgawanyo huu kwa sasa unalenga mgawanyo wa jimbo kuwa majimbo mawili, bado tutaendelea kuwa na halmashauri moja kwa maana ya utoaji huduma kwa ngazi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Jiji litaendelea kuwajibika katika utoaji wa huduma katika majimbo yote mawili”.
Akizungumzia kuhusu mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, alisisitiza kuwa, mgawanyo huo utazingatia zaidi kata na sio tarafa. “Kwa minajili ya jambo letu la leo la kupendekeza mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, tutaangalia zaidi kata na wakati utakapofika kutoa mapendekezo ya mgawanyo wa tarafa na mtaa kwa mamlaka zile basi tutarejea tena katika utaratibu wa kawaida” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Sambamba na hilo, alitoa rai kuwa, baraza lijikite katika mipaka ambayo inatambulika kwa mujibu wa sheria “nilikuwa nashauri baraza lako lijikite katika mipaka ambayo kwa sasa inatambulika kwa mujibu wa sheria, kwamba tunazo kata 41 na mitaa 222. Hivyo, vingine kwa sasa bado hatuna. Kwahiyo, mipango yetu yote nashauri tuweze kujikita hapo na pale itakapopendeza taratibu nyingine zitaweza kufuatwa” alishauri Dkt. Sagamiko.
Mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini umezingatia hali ya kiuchumi ya jimbo hasa suala la ukusanyaji mapato, lengo ikiwa ni kuona maeneo yaliyopo juu kiuchumi hayamezi kiuwakilishi maeneo yaliyo chini kiuchumi.