Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imefanya ziara kutembelea ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Dodoma leo tarehe 12 Machi 2025 na kupongeza mafanikio yaliyofikiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Namtumbo Mheshimiwa Vita Kawawa amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali Salum Haji Othman kwa mafanikio makubwa ya ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa.
Kamati hiyo imelipongeza JWTZ kwa kukidhi vigezo vya ujenzi, ubora wa jengo na imeahidi kuendeleza ushirikiano ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Kwa upande wake Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali Salum Haji Othman ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa kwani ni mafanikio makubwa kwa JWTZ kuwa na Makao Makuu ya Jeshi yaliyojengwa kwa kiwango cha Kimataifa.
Aidha, baada ya kukagua maeneo mbalimbali ya ujenzi ikiwemo ofisi za Wizara ya Ulinzi na JKT, Kamati hiyo ilitembelea ujenzi wa hospitali Kuu ya Jeshi ya ngazi nne, inayoendelea kujengwa eneo la Msalato, Dodoma.