Kampuni za Kitanzania zimetakiwa kuomba kandarasi za ujenzi wa miradi inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa visiwani Comoro
Hayo yameelezwa wakati wa mazunguzo kati ya Balozi wa Tanzania, Comoro, Mhe. Saidi Yakubu na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Comoro, Bi Rejane Hugouneno De Vreyer yaliyofanyika Moroni Machi 12, 2025.
Bi. De Vreyer alimweleza Balozi Yakubu kuwa Shirika lake linafadhili miradi na programu zenye thamani takriban Euro Milioni 113 kwa mwaka katika sekta za Afya, Ujenzi, Tehama na pia kutoa ushauri katika maeneo ya mifumo ya kodi, bajeti na maboresho ya sera.
Alisema kuwa miradi yote hiyo hutolewa kwa kandarasi za kimataifa na kutoa mwaliko kwa kampuni za Kitanzania kuchangamkia fursa hizo.
Kwa upande wake, Balozi Yakubu alimweleza Bi De Vreyer kuwa Tanzania ina ushirikiano mkubwa na Comoro katika maeneo yote aliyoyazungumzia na kwa hivi sasa wamekwishaanza kualika kampuni za Kitanzania kuchangamkia fursa za zabuni zinazotangazwa visiwani Comoro.